BIBI WA MIAKA 69 AUAWA KIKATILI BUNAMBIYU, KICHWA KIKIKATWA.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi.

Na Mwandishi wetu, Shy.

Kijiji cha Bunambiyu, wilaya ya Shinyanga Mkoa wa Shinyanga, pamegubikwa na hofu na mshtuko baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 69, Hollo Ruchanganya, kuuawa kikatili na mtu asiyejulikana. 

Imeelezwa kwamba, Mwili wake ulipatikana usiku wa Aprili 3, 2026, shambani mwa mahindi jirani na makazi yake, ukiwa kimekatwa kichwa – tukio linaloashiria unyama usiokuwa na kifani.


Taarifa za awali zinaonyesha kwamba mgeni ambaye bado hajafahamika alifika nyumbani kwa marehemu majira ya saa 3:00 usiku. Alikula pamoja na marehemu na wajukuu wake, kisha marehemu alimpeleka kwa mtalaamu wa tambiko la kuzuia kupata watoto pacha.


Baada ya muda mfupi, mgeni huyo alirudi nyumbani, akirejesha tochi na kuwataarifu wajukuu wa marehemu kwa maneno ya kutisha: "Bibi huyo atarejea asubuhi kutoka kwa mganga ambaye ni mama yake mdogo."


Asubuhi, mjukuu wa marehemu alipokuwa akielekea shambani aliona damu nyingi na nguo za marehemu. Alifahamisha ndugu wa marehemu, ambao walipofuatilia shamba hilo, waliukuta mwili wa Hollo Ruchanganya ukiwa umetupwa shambani, kichwa kikiwa kimekatwa kwa mapanga.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kikatili. Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mauaji hayo yana uhusiano na imani za kishirikina. Watu wawili tayari wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi.


Tukio hili limeacha jamii ya Bunambiyu kikiwa na hofu kubwa, huku wakazi wakihimizwa kuwa makini na wageni wanaoingia nyumbani usiku. Tukio hili linatufundisha kuwa tahadhari ni muhimu, hata ndani ya maeneo yanayojulikana.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments