ASILIMIA 32 YA WATOTO MASWA WANA UDUMAVU .

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano (wa pili kushoto aliye mbele) akikabidhi kitanda mmoja wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa na kanisa la TAG mjini Maswa.Picha na Samwel Mwanga  


Samwel Mwanga, Maswa.

MKUU wa Wilaya ya Maswa,  Mkoani Simiyu, Dk. Vicent Naano, amesema tatizo la udumavu kwa watoto katika wilaya hiyo bado ni kubwa, ambapo takribani asilimia 32 ya watoto wanakabiliwa na udumavu, hali inayohitaji juhudi zaidi katika utoaji wa elimu ya lishe kwa jamii.

Akizungumza Aprili 4, 2026 katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) mjini Maswa wakati akikabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu amesema serikali kwa kushirikiana na wataalamu wa afya, viongozi wa dini na jamii itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya lishe ili kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa lishe bora kwa watoto.

Amesema bado kuna upungufu wa elimu kuhusu makuzi na malezi ya awali kwa watoto, hususan katika suala la lishe, hali inayochangia kuendelea kuwepo kwa changamoto ya udumavu.


Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano akizungumza na waumini wa kanisa la TAG mjini Maswa wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.Picha na Samwel Mwanga.

Ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo, serikali imekuwa ikisisitiza wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupatiwa chakula wanapokuwa shuleni ili kusaidia kuboresha afya na maendeleo yao.

“Tutahakikisha elimu ya lishe inaendelea kutolewa kupitia mikutano ya vijiji, vituo vya afya na taasisi mbalimbali zikiwemo madhehebu ya dini. Viongozi wa dini pia mtusaidie kulisemea jambo hili ili kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto katika wilaya yetu,” amesema.

Baadhi ya wananchi wilayani humo wamesema bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya lishe katika ngazi ya familia ili kuwasaidia wazazi kuelewa umuhimu wa lishe bora kwa watoto.

Felister Mhoja, mkazi wa mtaa wa Majengo mjini Maswa, amesema wazazi wengi hawapati elimu ya kutosha kuhusu aina ya vyakula vinavyofaa kwa watoto.

“Watu wengi wanajua tu kumpa mtoto ugali na mboga, lakini hawajui umuhimu wa vyakula vingine kama mayai, maziwa na matunda kwa ukuaji wa mtoto,” amesema.

Kwa upande wake, Catherine John amesema baadhi ya wazazi wanakosa uelewa wa namna ya kuandaa mlo kamili kwa watoto licha ya vyakula kupatikana katika mazingira yao.

“Wakulima wengi tunalima mazao mbalimbali, lakini hatujui namna ya kuyachanganya ili mtoto apate lishe bora. Elimu ikitolewa zaidi itasaidia sana,” amesema.

Naye Elisha Ndalo, mkazi wa mjini Maswa, amesema utoaji wa elimu ya lishe kupitia vituo vya afya na mikutano ya vijiji unaweza kusaidia kupunguza tatizo hilo.

“Wazazi wengi wakielimishwa wataanza kubadilisha namna ya kuandaa chakula cha watoto wao,” amesema.

Sehemu ya Vitanda na magodoro vilivyotolewa na kanisa la TAG mjini Maswa kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.Picha na Samwel Mwanga.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki, amesema katika kukabiliana na tatizo la udumavu, serikali inaendelea kutoa elimu ya lishe kupitia vituo vya afya, kliniki za watoto na kampeni mbalimbali za afya ili kuongeza uelewa kwa wazazi.

Amesema udumavu kwa watoto mara nyingi husababishwa na ukosefu wa lishe bora katika kipindi cha miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto, hivyo wazazi wanapaswa kuzingatia mlo kamili unaojumuisha vyakula vya aina mbalimbali.

“Ushirikiano wa wazazi, viongozi wa jamii na wataalamu wa afya ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora inayochangia ukuaji wao wa mwili na akili,” amesema.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments