WIZI WA VIUADUDU VYA PAMBA MASWA WAFICHULIWA.

 

Baadhi ya chupa za viuadudu vya zao la pamba aina ya BATAMU 175 EC zilizodaiwa kuibiwa katika ghala la Amcos ya Masamwa katika kijiji cha Ishima wilaya ya Maswa na kutelekezwa.(Picha na Samwel Mwanga).

-DC,Vicent Naano aagiza mtuhumiwa akamatwe.

Samwel Mwanga, Maswa.

KATIBU  wa Chama cha Ushirika wa Msingi (AMCOS) cha Masanwa katika Kijiji cha Ishima, Kata ya Bugarama wilayani Maswa mkoani Simiyu, Paul Robert, anadaiwa kuhusika na wizi wa viuadudu vya zao la pamba vyenye thamani ya Sh 23 milioni  mali ya Serikali.

Viuadudu hivyo vilivyokuwa na jumla ya chupa 1,300 vinatajwa kuwa ni aina ya Batamu 175EC (Box 3) na 44EC (Box 7), ambavyo vililetwa na Bodi ya Pamba Tanzania kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima wa pamba katika kijiji hicho ili kukabiliana na wadudu wanaoshambulia zao hilo.

Tukio hilo limebainika baada ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano, kufika katika kijiji hicho na kushuhudia chupa 1,190 za viuadudu hivyo zikiwa zimetelekezwa katika kichaka kilichopo umbali wa takribani mita 500 kutoka nyumbani kwa mtuhumiwa.

Akizungumza leo Machi 25,2026 Dc Naano amesema tayari amelielekeza Jeshi la Polisi wilayani Maswa kumsaka mtuhumiwa huyo ili akamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

“Hili ni suala zito kwa sababu hizi ni mali ya Serikali zilizokusudiwa kuwasaidia wakulima. Nimeagiza polisi wamsake mtuhumiwa popote alipo ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano (wa pili kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Ishima kwenye eneo ambalo zilikutwa chupa za viuadudu wa zao la pamba zilizodaiwa kuibiwa.Picha na Samwel Mwanga.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ishima, Lucas Mwakimwadoto, amesema viuadudu hivyo vilipokelewa kijijini hapo machi 19,2026  vikiletwa na Bodi ya Pamba kwa ajili ya kugawiwa wakulima, lakini baadaye iligundulika kuwa vina upungufu.

“Hizi dawa zilipotea katika mazingira ambayo binafsi siyafahamu. Taarifa ya awali niliipata kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji, lakini baadaye tukapata taarifa kuwa chupa 1,190 zimepatikana kwenye kichaka karibu na makazi ya mtuhumiwa ambaye baada ya tukio hilo alitoweka na hajulikani alipo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk, amesema walisambaza viuadudu hivyo baada ya kubaini mashambulizi makubwa ya wadudu katika mashamba ya pamba.

Amesema hatua hiyo ililenga kuokoa zao hilo ili wakulima wasipate hasara katika msimu huu wa kilimo.


Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano (kulia) akiangalia moja ya chupa ya viuadudu vya zao la pamba vilivyoibiwa na kutelekezwa katika kijiji cha Ishima wilaya humo, kushoto ni Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk,  Picha na Samwel Mwanga.

Naye Kaimu Afisa Kilimo wa Wilaya ya Maswa, Diana Lyimo, amesema tukio hilo limeathiri uzalishaji wa zao la pamba katika eneo hilo.

Amesema zaidi ya hekari 13,000 za pamba katika kijiji hicho ziko hatarini kutopuliziwa kwa wakati kutokana na kuchelewa kwa dawa hizo kufika kwa wakulima.

“Kuchelewa kwa viuadudu hivi kunaweza kuathiri uzalishaji wa pamba kwa kiwango kikubwa kwa sababu wadudu hushambulia zao hili kwa kasi,” amesema Lyimo.

Baadhi ya wakulima wa pamba katika kijiji hicho wameeleza wasiwasi wao wakihofia kupoteza mavuno kutokana na kuchelewa kwa dawa hizo.

Mkulima Sengerema Mwandu amesema kuchelewa kwa viuadudu hivyo kunaweka hatarini mavuno ya wakulima wengi.

“Pamba tayari imeanza kushambuliwa na wadudu. Bila dawa hizi kwa wakati tunaweza kupata hasara kubwa sana,” amesema.

Baadhi ya chupa za viuadudu vya zao la pamba aina ya TAKE 44EC zilizodaiwa kuibiwa katika ghala la Amcos ya Masamwa katika kijiji cha Ishima wilaya ya Maswa na kutelekezwa.Picha na Samwel Mwanga

Naye Jilala Mahega, mkulima mwingine wa pamba katika kijiji hicho, amesema wakulima wamekuwa wakitegemea msaada huo wa serikali ili kuokoa mashamba yao.

“Serikali ilitusaidia kwa kutuletea dawa hizi, lakini tukisikia zimepotea tunapata hofu kwa sababu pamba ndiyo tegemeo letu kubwa la kipato,” amesema.

Jeshi la Polisi wilayani Maswa linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments