Na Samwel Mwanga, Simiyu.
ZAIDI ya watoto 837,038 wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya ugonjwa wa polio katika mkoa wa Simiyu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuendelea kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo hatari unaosababisha ulemavu wa kudumu kwa watoto.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 17, 2026, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Boniphace Marwa amesema kuwa zoezi hilo la chanjo litafanyika kwa siku nne kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026, likihusisha watoto wote waliopo kwenye kundi lengwa bila kujali kama walishawahi kupata chanjo hapo awali.
“Lengo la kampeni hii ni kuhakikisha tunalinda watoto wetu dhidi ya ugonjwa wa polio ambao hauna tiba, lakini unaweza kuzuilika kwa chanjo. Tunawahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo hii kwa wakati,” amesema Dk. Marwa.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Boniface Marwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya zoezi la chanjo ya.polio ambalo litaanza kutolewa Machi 24 hadi 27,2026 kwa watoto chini ya miaka 10 mkoani humo.Picha na Samwel Mwanga.Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Simiyu, Beatrice Kapufi amesema kuwa jumla ya vituo 1,899 vitawekwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa watoto wote.
“Mbali na vituo vya kutolea huduma, pia kutakuwa na timu za wahudumu wa afya zitakazokwenda nyumba kwa nyumba pamoja na kufika katika maeneo ya mikusanyiko ya watu kama masoko, shule na maeneo ya ibada ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo,” amesema .
.
Ameongeza kuwa maandalizi ya kampeni hiyo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa chanjo, vifaa tiba na mafunzo kwa wahudumu wa afya watakaoshiriki katika zoezi hilo.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha jamii ili kufanikisha kampeni hiyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesema kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kupunguza maambukizi ya polio duniani, bado kuna umuhimu wa kuendelea kutoa chanjo ili kuzuia uwezekano wa kurejea kwa ugonjwa huo.
Neema Rubein ni mtangazaji wa kituo cha radio ya kijamii ya Bariadi Fm iliyoko mjini Bariadi amesema kuwa mafunzo yamemfanya kupata elimu juubya ugonjwa huo.
“Baada ya mafunzo haya, tumeelewa kwa kina umuhimu wa kuelimisha jamii kuhusu chanjo ya polio. Sisi kama waandishi wa habari tutahakikisha tunatoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo.”amesema.
Constantine Mathias ambaye ni mwandishi wa gazeti la Uhuru amesema kuwa kupitia mafunzo hayo amefahamu madhara ya ugonjwa huo.
“Mafunzo haya yametusaidia kufahamu madhara ya polio na namna inavyozuilika. Tutaandika habari zenye kuelimisha na kuondoa upotoshaji wowote unaoweza kujitokeza kuhusu chanjo hii.”amesema.
Naye Shaban Lupimo ambaye ni mwandishi wa habari wa kituo cha Star TV ammelezq jinsi atakavyotumia chombo chake cha habari kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya ugonjwa huo.
"Tutatumia vyombo vyetu kufikisha ujumbe kwa jamii kwa njia rahisi na inayoeleweka. Ni muhimu kila mzazi akatambua kuwa chanjo ya polio ni salama na ni kinga ya maisha kwa mtoto.”amesema.
MWISHO.






0 Comments