Na Samwel Mwanga,Maswa
Kikundi cha Wanawake na Samia mkoani Simiyu kimetoa vyerehani 10 kwa wanawake wa kikundi hicho katika wilaya ya Maswa ikiwa ni sehemu ya mpango wa kusambaza vyerehani 50 kwa wanawake wenye lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za ushonaji.
Akikabidhi vyerehani hivyo kwa wanufaika, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wilaya ya Maswa, Shukurathi Kachwambwa amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuwapa fursa ya kujiajiri badala ya kutegemea kipato cha watu wengine.
Amesema vyerehani hivyo vinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta tija kwa wanachama wa kikundi hicho na jamii kwa ujumla.
“Tunatarajia vyerehani hivi viwe chachu ya kuanzisha na kuimarisha shughuli za ushonaji kwa wanawake wetu. Hii itawasaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu,Mwanahawa Said Maswa, amewataka wanufaika kuvitunza vyerehani hivyo na kuhakikisha vinatumika kwa bidii ili kufikia lengo la kuinua uchumi wa wanawake.
Amesema kuwa kikundi hicho kinaendelea kutafuta fursa mbalimbali za kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia miradi midogo midogo ya uzalishaji.
“Ninawasihi wanufaika kutumia vyerehani hivi kwa uaminifu na kujituma katika kazi ili mradi huu uwe mfano mzuri na uweze kuwasaidia wanawake wengine kupata fursa kama hizi,” amesema.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Maswa, Fredrick Mussa, amesema uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni moja ya njia muhimu za kupunguza umaskini katika jamii na kuimarisha ustawi wa familia.
Amesema serikali inaendelea kuhimiza vikundi vya wanawake kutumia vizuri fursa wanazopewa ili kuweza kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii.
“Tunawahimiza wanawake kuendeleza ujuzi wa ushonaji na kushirikiana kama kikundi ili kuhakikisha mradi huu unaleta matokeo chanya kwa wanachama wote,” amesema.
Baadhi ya wanufaika wa vyerehani hivyo wameeleza kufurahishwa na msaada huo wakisema utawasaidia kuanza au kupanua shughuli zao za ushonaji.
Mwanakikundi Metlida Masanja amesema awali alikuwa na ujuzi wa ushonaji lakini alikosa mtaji wa kununua cherehani, hivyo msaada huo utamwezesha kuanzisha kazi na kujipatia kipato
“Nilikuwa na ndoto ya kuwa na cherehani yangu lakini sikuwa na uwezo wa kuinunua. Sasa nitaanza kushona nguo na kupata kipato cha kusaidia familia yangu,” amesema.
Naye Rehema Alfa, ambaye pia ni mnufaika wa cherehani hiyo, amesema ataitumia kujiajiri na kuwafundisha wanawake wengine ujuzi wa ushonaji ili nao waweze kujitegemea kiuchumi.
Mpango wa kugawa vyerehani 50 kwa wanawake wa mkoa wa Simiyu unatarajiwa kusaidia kuongeza fursa za ajira kwa wanawake pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii.
MWISHO.











0 Comments