WANAWAKE NA SAMIA SIMIYU WAREJESHA TABASAMU KWA MAMA MATHIAS.

 

Restuta Ernest (kushoto) akimkabidhi msaada wa mahindi Eva Elias (kulia) yaliyotolewa na Kikundi cha Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

KIKUNDI cha Wanawake na Samia Mkoa wa Simiyu kimetoa msaada wa vitu mbalimbali pamoja na fedha taslimu kwa mkazi wa Mnadani wilayani Maswa, Eva Elias maarufu kama Mama Mathias, anayekabiliwa na changamoto za maisha.

Msaada huo umetolewa baada ya wanakikundi hicho kubaini hali ngumu ya maisha ya familia hiyo kupitia mwanafunzi Mathias Emanuel anayesoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyalikungu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo nyumbani kwa mama huyo, kiongozi wa msafara wa kikundi hicho, Restuta Ernest, amesema waligundua hali ya mwanafunzi huyo wakati walipofika wilayani humo kutoa misaada ya madaftari na kalamu kwa wanafunzi wa shule za msingi kutoka familia zisizojiweza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu.

Amesema wakati wa zoezi hilo walisikitishwa na hali ya mwanafunzi huyo aliyefika kupokea vifaa vya shule akiwa amevaa sare yenye viraka hali iliyowagusa na kuwafanya kufuatilia zaidi maisha yake.

Rehema Alfa (kushoto) mwanachama wa kikundi cha Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu akimkabidhi simu Eva Elias (kushoto) iliyotolewa na kikundi ikiwa ni sehemu ya misaada waliyompatia.

“Katika wanafunzi waliokuja kupokea vifaa vya shule, Mathias alifika akiwa amevaa sare yenye viraka. Hali hiyo ilitugusa sana na kuamua kufuatilia zaidi kwa kufika nyumbani kwao. Tulipofika ndipo tuligundua familia hiyo inaishi katika mazingira magumu,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, wanakikundi waliamua kutoa msaada mbalimbali ikiwemo mahindi, mchele, maharagwe, mafuta ya kula, sabuni za kufulia, nguo za familia, cherehani moja, simu ya mkononi pamoja na fedha taslimu Sh110,000 ili kumsaidia mama huyo kujikwamua kiuchumi.

Mwanachama wa kikundi hicho, Betrice Ngassa, amesema walipofika nyumbani kwa familia hiyo waligundua mahitaji makubwa ni chakula na msaada wa kumwezesha mama huyo kujipatia kipato.

“Wanawake tunaongozwa na moyo wa huruma. Leo tumefika hapa kumtia moyo mama mwenzetu na tunatumaini msaada huu utakuwa chachu kwake kujishughulisha na kujiongezea kipato,” amesema.

Kwa upande wake, Mama Mathias ameishukuru kikundi hicho kwa msaada waliompatia akisema utamsaidia kuanza kujishughulisha ili kuimarisha maisha ya familia yake.

“Nawashukuru sana wanawake wenzangu kwa kunikumbuka katika hali yangu. Msaada huu utanipa nguvu ya kuanza kujishughulisha ili niweze kuihudumia familia yangu,” amesema.

Eva Elias (Maarufu Mama Mathias) alizungumza mara baada ya kupokea misaada mbalimbali iliyotolewa na kikundi cha Wanawake na Samia mkoa wa Simiyu.

Naye mwanafunzi Mathias Emanuel amesema msaada huo umempa faraja kubwa huku akiahidi kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zake na kuweza kumsaidia mama yake siku za baadaye.

“Mimi nashukuru sana kwa msaada huu. Naahidi kusoma kwa bidii ili siku moja niweze kumsaidia mama yangu na familia yetu,” amesema.

Mwanafunzi Mathias Emanuel wa darasa la saba shule ya msingi Nyalikungu wilaya ya Maswa akizungumza mara baada ya familia yao kupatiwa misaada mbalimbali na kikundi cha wanawake na Samia mkoa wa Simiyu.

Wananchi wazungumzia msaada huo Mkazi wa  Mwawayi mjini Maswa, Juma Magesa, amesema kitendo cha wanawake hao kuifikia familia hiyo ni mfano mzuri wa mshikamano wa kijamii.

“Ni jambo jema sana kuona watu wanaguswa na matatizo ya wengine. Msaada kama huu unaweza kubadili maisha ya familia ambayo ilikuwa inapitia wakati mgumu,” amesema 

Naye Mwenyekiti wa kitongoji hicho,Anania Batungi, ambaye pia alimfahamu mwanafunzi huyo, amesema msaada huo utamsaidia mwanafunzi huyo kupata mazingira bora ya kujifunza.

“Mathias ni mwanafunzi mwenye bidii lakini changamoto za nyumbani zilikuwa zinaonekana. Msaada huu utampa motisha zaidi ya kuendelea kusoma kwa juhudi,” amesema.

Utoaji wa misaada hiyo ni sehemu ya jitihada za kikundi cha Wanawake na Samia mkoani Simiyu kusaidia makundi yenye uhitaji na kuhamasisha wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.

MWISHO. 






Post a Comment

0 Comments