TMDA: WAKAGUZI WA DAWA WASIJIGEUZE POLISI.

 Mkaguzi Mwandamizi wa TMDA kanda ya Ziwa Mashariki,Venance Burushi akizungumza wakati wa mafunzo kwa wakaguzi wa dawa katika halmashauri za wilaya za mkoa wa Simiyu yaliyofanyika wilayani Maswa.Picha na Samwel Mwanga.

Samwel Mwanga, Maswa

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imewataka wakaguzi wa dawa katika halmashauri kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za ukaguzi wa maduka ya dawa muhimu na ya mifugo badala ya kujigeuza kuwa maafisa wa ukamataji au polisi.

Wito huo umetolewa leo Machi 30, 2026 na Mkaguzi Mwandamizi wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Venance Burushi, wakati akizungumza katika mafunzo kwa wakaguzi wa dawa kutoka halmashauri za wilaya mbalimbali za mkoa wa Simiyu yaliyofanyika wilayani Maswa.

Amesema wakaguzi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria za ukaguzi na kutoa elimu kwa wahudumu wa maduka ya dawa pamoja na jamii, badala ya kutumia vitisho au mabavu.


Amesema katika utekelezaji wa majukumu yao ni muhimu kushirikiana na taasisi nyingine za serikali ambazo zina mamlaka ya kisheria ya kukamata wahalifu na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

“Kukamata na kuwafunga watu kamba mikononi hayo si majukumu yenu. Ukimkuta mtu amefanya kosa usijigeuze askari polisi wala usijifanye mbabe, badala yake unapaswa kutoa elimu kwa jamii,” amesema.

Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Deogratius Mtaki akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa wakaguzi wa dawa katika halmashauri za wilaya za mkoa wa Simiyu yaliyofanyika wilayani Maswa.Picha na Samwel Mwanga.

Ameongeza kuwa wakaguzi wana nyenzo mbalimbali za kisheria zinazowaongoza katika utendaji wao wa kazi, ikiwemo sheria na kanuni za ukaguzi wa dawa na vifaa tiba

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki, amesema maadili ni jambo muhimu kwa mkaguzi wa dawa ili kuhakikisha bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA zinakuwa salama kwa matumizi ya wananchi.

Amesema mkaguzi mwenye maarifa lakini asiyezingatia maadili anaweza kuhatarisha afya ya jamii kwa kuruhusu bidhaa duni au bandia kuingia sokoni.

“Kuwa na maarifa pekee bila maadili ni sawa na kutokuwa na maarifa, kwa sababu kukosa maadili kunaweza kusababisha mkaguzi kuruhusu bidhaa duni au bandia kuingia au kuwepo sokoni,” amesema.

Baadhi ya wakaguzi wa dawa katika halmashauri za wilaya za mkoa wa Simiyu wakiwa katika mafunzo yaliyotolewa na TMDA.Picha na Samwel Mwanga.

Kwa upande wake, Faudhia Jungu, mkaguzi wa dawa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria za ukaguzi ili kuepuka kuleta taharuki kwa jamii wakati wa ukaguzi wa maduka ya dawa.

Naye Faida Manila, mkaguzi wa dawa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, amesema moja ya changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ni ukosefu wa bajeti ya kutosha katika halmashauri kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa maduka ya dawa.

Amesema hali hiyo wakati mwingine huwafanya washindwe kufika katika maeneo yote yanayohitaji ukaguzi, jambo linaloweza kuathiri udhibiti wa ubora wa dawa katika jamii.

Mwisho.




Post a Comment

0 Comments