DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Kairuki, amezindua rasmi mfumo wa kidijitali wa kuhudumia watumiaji wa huduma za mawasiliano ujulijanao kama Mtumiajiapp ulioandaliwa na TCRA-CCC wenye lengo la kuboresha mifumo ya mawasiliano nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo leo Machi 23,2026 katika ukumbi wa Millennium Towers uliopo jijini Dar es Salaam , Waziri Kairuki amesema kuwa uzinduzi wa mfumo huo ni hatua muhimu katika kuboresha na kurahisisha huduma za mawasiliano.
Ameeleza kuwa mfumo huo utasaidia watumiaji kupata taarifa muhimu, elimu ya matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano pamoja na kutoa nafasi ya kuwasilisha changamoto na maoni yao.
Waziri Kairuki amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024 hadi 2034 uliozinduliwa na Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkakati huo unalenga kuongeza uelewa wa matumizi ya teknolojia na kuhakikisha wananchi wanatumia mifumo ya kidijitali kwa usalama na ufanisi.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), idadi ya laini za simu imeongezeka na kufikia Milioni 106.9 hadi Desemba 2025, huku watumiaji wa Intaneti wakifikia Milioni 58.6. Ongezeko hilo linaonesha kukua kwa kasi kwa sekta ya mawasiliano nchini.
Serikali pia imeendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo jumla ya minara 758 imejengwa na kufikisha huduma katika vijiji zaidi ya 1,400. Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi zaidi kupata huduma za mawasiliano hata katika maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
Pamoja na mafanikio hayo, Waziri Kairuki alitaja changamoto zinazokabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa watumiaji, uvunjifu wa faragha, pamoja na vitendo vya utapeli mtandaoni. Alisema mfumo wa Mtumiaji utasaidia kushughulikia changamoto hizo kwa kutoa njia rahisi ya kuwasiliana na wadau husika.




0 Comments