Mhandisi Abdulkarim Mariki akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya ofa walizotoa kwa wateja wao ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya maji mwaka 2026.Na Samwel Mwanga,Maswa.
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) mkoani Simiyu imetangaza ofa maalum kwa wateja wake katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa mwaka 2026, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mhandisi Abdulkarim Mariki kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA amesema ofa hizo zinahusisha kuondoa gharama ya kurejeshewa huduma ya maji kwa wateja waliokuwa wamekatwa huduma pamoja na kuruhusu wateja wenye madeni makubwa kulipa kwa awamu hadi watakapomaliza.
Amesema ofa ya kuondoa gharama ya kurejeshewa huduma itadumu hadi Aprili 16, 2026, huku akiwahimiza wananchi kuitumia fursa hiyo kurejesha huduma zao.
"Ofa ya kuondoa gharama ya kurejeshewa huduma itakuwa ndani ya siku 30 yaani kuanzia Machi 16 hadi April 16,2026 hivyo wateja wachangamkie fursa hiyo,'amesema.
Amesema katika kipindi cha maadhimisho hayo, yanayotarajiwa kufikia kilele machi 22, 2026, mamlaka hiyo imeandaa hema maalum nje ya ofisi zake kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja, akiwataka wenye changamoto mbalimbali kujitokeza ili zipatiwe ufumbuzi.
Mtumishi wa Mauwasa,Queen (kushoto) akimsikiliza mteja aliyefika kwenye hema kwa ajili ya kutatua changamoto ya ulipaji deni la maji ambalo ninla muda mrefu.Baadhi ya wateja wa mamlaka hiyo wameipokea ofa hiyo kwa hisia tofauti, wakieleza namna inavyogusa maisha yao ya kila siku.
Mkazi wa Maswa Mjini, Rehema Joseph, amesema hatua ya kuruhusu ulipaji wa madeni kwa awamu itasaidia wananchi wengi waliokuwa wamelemewa na bili kubwa.
“Tulikuwa tunapata changamoto kulipa madeni kwa mkupuo, lakini hii nafasi ya kulipa kidogo kidogo itatusaidia kurejea kwenye huduma ya maji bila presha kubwa,” amesema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara katika eneo la soko la Maswa, Juma Said, amesema ujio wa mita za malipo kabla utasaidia kudhibiti matumizi na kuepuka migogoro ya bili.
“Hizi mita za kulipia kabla zitatusaidia kupanga matumizi yetu. Unatumia kadri ya uwezo wako, tofauti na sasa ambapo bili zinakuja kubwa bila kutarajia,” amesema .
Naye Beatrice Michael, mkazi wa kata ya Zanzui ameipongeza MAUWASA kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia hema maalum.
“Kuweka hema nje ya ofisi ni jambo zuri, watu wengi walikuwa wanaogopa kufika ofisini. Sasa tutapata nafasi ya kueleza changamoto zetu kwa urahisi,” amesema.
Hatua ya MAUWASA kuja na ofa hiyo inaonekana kuwa sehemu ya juhudi za serikali na mamlaka zake kuboresha huduma ya maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.
Mwisho.






0 Comments