MAUWASA YABAINI WIZI WA MAJI MJINI MASWA.

 Mita ya maji namba 2023061246 ya Mauwasa ambayo ilikuwa ikitumiwa na Haruna Mahamood wa mtaa wa Unyanyembe mjini Maswa iliyositishiwa huduma kutokana na deni.Picha na Samwel Mwanga

 Samwel Mwanga, Maswa

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Maswa (Mauwasa) imeonya wananchi wanaojiunganishia huduma ya maji kinyume cha utaratibu kuacha mara moja tabia hiyo, ikisema itachukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika.

Onyo hilo limetolewa leo Machi 26,2026 na Mhandisi wa mamlaka hiyo, Abdulkarim Marik baada ya kumkamata mkazi wa mtaa wa Unyanyembe mjini Maswa, Haruna Mahamood  akidaiwa kujiunganishia maji kinyume cha utaratibu na kutumia huduma hiyo kwa takribani miezi mitatu bila kulipia huku akiuza maji hao kwa majirani zake.

Mhandisi Marik amesema ukaguzi uliofanywa na wataalamu wa mamlaka hiyo ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alisitishiwa huduma kwa kushindwa kulipa deni lake alikuwa ameunganisha bomba la maji nyuma ya mita ya maji na hivyo kutumia bila kulipia.

Mhandisi wa Mauwasa, Abdulakarim Marik alizungumza mara baada ya kubaini wizi wa maji katika nyumba ya Haruna Mahamood mkazi wa Unyanyembe mjini Maswa.Picha na Samwel Mwanga.

“Tumebaini kuwa alifanya muunganisho huo kinyume cha taratibu na kwa muda wa takribani miezi mitatu alikuwa akitumia maji bila kulipia na mbaya zaidi amekuwa akiuza maji kwa majirani zake. Hili ni kosa kisheria na tutachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” amesema.

Amesema vitendo vya wizi wa maji vinaathiri mapato ya mamlaka hiyo na pia kusababisha upotevu wa maji ambao unaweza kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengine.

Mhandisi Marik amesema kuwa amewataka wananchi wanaohitaji huduma ya maji kufuata taratibu rasmi za kuomba kuunganishiwa huduma hiyo badala ya kufanya miunganisho isiyo halali.

“Tunatoa rai kwa wananchi wote wanaohitaji huduma ya maji kufika ofisini kwetu ili kupata muunganisho halali. Kujichukulia hatua za kuunganisha maji kinyume cha utaratibu ni kosa na hatua kali zitachukuliwa,” ameongeza.

Amessema kuwa itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini miunganisho isiyo halali na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Baadhi ya wananchi wa Maswa wamepongeza hatua hiyo wakisema itasaidia kudhibiti upotevu wa maji na kuongeza uwajibikaji katika matumizi ya huduma hiyo.

Suzana John ni mkazi wa mtaa wa Unyanyembe mjini humo amesema kudhibiti wizi wa maji ni muhimu kwa kuwa kuna wananchi wengi wanaolipia huduma hiyo kwa uaminifu.

“Ni vizuri mamlaka kuchukua hatua kwa wanaoiba maji kwa sababu sisi tunaolipa bili tunapata hasara. Kama kila mtu atafuata utaratibu huduma itakuwa bora zaidi,” amesema.

Naye Juma Ally, mkazi mwingine wa Maswa, amesema vitendo vya kujiunganishia maji kiholela vinaweza pia kusababisha uharibifu wa miundombinu ya maji.

“Watu wanapounganisha maji kienyeji wanaharibu mabomba na wakati mwingine maji yanapotea bila sababu. Serikali ikisimamia hili vizuri huduma itaimarika,” amesema.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments