Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Sospeter Mtwale, akifungua mafunzo ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji.Na Fadhili Abdallah, Kigoma
MADIWANI katika halmashauri za wilaya, mijiji na majiji nchini wametakiwa kutokuwa chanzo cha vurugu zinazoweza kuchangia kuzorotesha mahusiano baina ya watendaji na madiwani na kukwamisha shughuli za maendeleo nchini na ukusanyaji mapato.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Sospeter Mtwale alisema hayo akifunga mafunzo kwa madiwani wa Halmshauri ya wilaya Kigoma na manispaa ya Kigoma Ujiji ikiwa ni hitimisho la mafunzo kwa wajumbe wa mabaraza ya madiwani katika halmashauri 184 nchini.
Mtwale alisema kuwa madiwani wanapaswa kuwa kichocheo katika kubuni, kusimamia utekelezaji wa shughuli za maendeleo za halmashauri, kuchochea ukusanyaji mapato na kusimamia rasilimali watu, fedha na rasilimali zilizopo kwenye hamashauri ikiwemo rasilimali ardhi ambayo ndiyo msingi wa rasilimali kuu ya halmashauri.
Kufuatia mafunzo hayo Kiongozi huyo alisema kuwa mafunzo hayo yatawajenga madiwani kujua majuku, wajibu na mipaka ya utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo kujua mipaka na viwango vya stahiki zao na kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo madiwani watakuwa chachu kubwa ya kuleta maendeleo kwenye halmashauri zao.
Akieleza madhumuni ya mafunzo hayo yaliyotolewa na chuo ch serikali za mitaa Hombolo, Mkuu wa chuo hicho,Dk.Yusuph Mashala alisema kuwa mafunzo yalilenga kuwajengea uwezo madiwani kujua wajibu, majukumu, mipaka ya utendaji wao na nafasi yao katika kuchochea maendeleo kwenye halmashauri zao na jukumu la kusimamia maendeleo, ukusanyaji wa mapato na matumizi ya halmashauri.




0 Comments