JESHI la Polisi mkoani Mtwara limemkamata kijana Ibrahimu Mugendi kwa tuhuma za kukusanya michango isivyo halali baada ya kujifanya bubu akidai anahitaji msaada.
Mtuhumiwa huyo, Mugendi, mkazi wa Mkoa wa Kigoma, anadaiwa kujifanya ana tatizo la kuongea ili kuomba michango kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali, kabla ya kufichuliwa na kukamatwa na polisi.
Akizungumza na SAKAGOI BLOG leo Machi 27, 2026, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Issa Suleiman amesema mtuhumiwa aliwasili mkoani humo Februari 18, 2026 na kufikia katika moja ya nyumba za kulala wageni.
Kamanda Suleiman amesema siku chache baadaye, Februari 26, mtuhumiwa alifika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kuomba kibali cha kuchangisha fedha, akidai anahitaji msaada kutokana na changamoto ya kiafya inayomfanya ashindwe kuongea.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kamanda huyo, uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa hakuwa na tatizo lolote la kuongea, bali alitumia mbinu ya kujifanya bubu ili kujipatia fedha kutoka kwa wananchi..

0 Comments