WAANDISHI WA HABARI 64 WAFUZU KUWANIA TUZO ZA SAMIA KALAMU 2026; WASHINDI KUPEWA TUZO DESEMBA 5 DAR.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza orodha ya waliofuzu hatua ya mwisho ya Tuzo za Samia Kalamu Awards 2026, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Peter Mwasyalanda, jijini Dar es Salaam, Novemba 17, 2026.

Na Mwandishi Wetu  MALUNDE 1 BLOG – Dar es Salaam

Waandishi wa habari 64 kutoka vyombo vya habari 11 wamefuzu kuingia hatua ya mwisho ya kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari za Maendeleo (Samia Kalamu Awards 2026), baada ya kazi 3,003 kuwasilishwa kushindanishwa katika tuzo hizo zinazolenga kutambua na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari za maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 17, 2026, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mhandisi Peter Mwasyalanda, ametangaza orodha ya waliofuzu na kueleza kuwa kati ya kazi 3,003 zilizowasilishwa, kazi 882 zilifuzu kupigiwa kura na wananchi.

Amesema katika hatua hiyo jumla ya kura 317,399 zilipigwa, huku waliofuzu hatua ya mwisho wakipatikana kupitia tathmini ya majaji 19 na kura za wananchi.

Ameeleza kuwa majaji walizingatia vigezo mbalimbali, vikiwemo ubora wa maudhui, uzingatiaji wa maadili ya taaluma, matumizi ya utafiti na takwimu, athari chanya kwa jamii pamoja na mchango wa kazi hizo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben, amesema uteuzi wa waliofuzu ulizingatia ubora wa kazi zilizowasilishwa na vigezo vilivyotangazwa kwenye tovuti rasmi ya tuzo hizo.

Dkt. Reuben amesema Kamati ya Maandalizi itawapatia waliofuzu maelekezo kuhusu ushiriki wao katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, huku orodha kamili ya waliofuzu ikipatikana kupitia tovuti rasmi ya Samia Kalamu Awards.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewashukuru waandishi wa habari kwa kushiriki katika mchakato huo na kuwataka kuendelea kuzingatia maadili, weledi na uwajibikaji katika kazi zao.

Amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi kwa kuzingatia viwango vya taaluma ni muhimu katika kuimarisha imani ya jamii kwa vyombo vya habari.

Hafla ya kuwatunuku washindi inatarajiwa kufanyika Desemba 5, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Post a Comment

0 Comments