
Na, Samwel Mwanga, Maswa.
KAMPUNI ya Sigara Tanzania (TCC) imetoa majiko ya gesi 300, vyerehani 70 vya umeme na jozi 50 za magongo ya kutembelea kwa watu wenye ulemavu wa miguu kupitia Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Akizungumza Oktoba 31 2026, katika kijiji cha Njiapanda, Kata ya Isanga, baada ya kupokea msaada huo, Mbunge Mashimba Ndaki ameishukuru kampuni hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika utunzaji wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema kuwa kupatikana kwa msaada huo unatokana na jitihada zake za kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuweza kumsaidia kwa ajili ya ustawi wa wananachi wa jimbo hilo kupitia makundi mablimbali ya kijamii.
Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki(kushoyo)akimkabidhi mtungi mdogo wa gesi ya kupikia,Suzana Masanza (kulia) katika kijiji cha Njiapanda. Picha na Samwel Mwanga“Wadau wetu wa maendeleo ambao ni kampuni ya TCC wametupatia majiko haya ya kupikia kwa mama na baba lishe wote wa jimbo hili na hizi ni jitihada za kuiunga mkono serikali katika suala la utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama,” amesema.
Amesema kuwa majiko hayo yatagawiwa kwa mama na baba lishe waliotambuliwa katika vijiji vya jimbo hilo, huku vyerehani vikipewa vikundi vilivyobainishwa, ambapo kila kikundi kitapata cherehani moja.
Amesema kuwa ofisi yake imeandaa utaratibu wa kuwafikishia wanufaika vifaa hivyo katika vijiji vyao ili kurahisisha upatikanaji wake.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza katika hafla ya ugawaji wa majiko ya gesi, vyerehani na magongo ya walemavu katika kijiji cha Njiapanda wilaya ya Maswa. Picha na Samwel MwangaKwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme, amesema serikali imekuwa ikiwawezesha wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa makundi maalumu, huku mbunge huyo akitafuta wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo.
Ngeme amewataka wanufaika kutumia msaada huo kuboresha maisha yao, akieleza kuwa majiko ya gesi yatawasaidia mama na baba lishe kupunguza muda wa kupika na kufanya shughuli zao katika mazingira bora.
“Majiko haya mliyopewa yatasaidia kutumia muda mfupi kupika vyakula. Gesi ikiisha mjaze. Hata hivi vyerehani ni vya kisasa vinavyotumia umeme, hivyo mnaweza kushona nguo nyingi kwa muda mfupi,” amesema.
Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki akizungumza katika hafla ya ugawaji wa majiko ya gesi, vyerehani na magongo ya walemavu katika kijiji cha Njiapanda wilaya ya Maswa. Picha na Samwel MwangaMwakilishi wa TCC, Edith Mkwama, amesema kuwa kampuni hiyo inatarajia msaada huo utatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwemo kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Suzana Masanza, mama lishe aliyenufaika na msaada huo, amesema kuwa gharama na umbali wa kufuata gesi ni miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kuwafanya baadhi ya wananchi kuacha kutumia nishati hiyo.
Amesema baadhi ya mama na baba lishe wanaoishi vijijini hulazimika kutumia muda mrefu kwenda mjini Maswa kujaza mitungi yao, hali inayoweza kuwafanya kurejea kwenye matumizi ya mkaa na kuni.
Mwakilishi wa kampuni ya TCC,Edith Mkwama akizungumza katika hafla ya ugawaji wa majiko ya gesi, vyerehani na magongo ya walemavu katika kijiji cha Njiapanda wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga“Changamoto kubwa ni gesi ikiisha. Wengi wetu tunaishi vijijini na tunatumia muda mrefu kwenda mjini Maswa kujaza mitungi. Hali hii inawafanya wengine kuitelekeza gesi na kurudia kutumia mkaa na kuni,” amesema.
Kwa upande wake, Monica Jilala, ambaye ni mwanakikundi wa Mshikamano Isanga kilichopatiwa cherehani, amesema kuwa msaada huo utawasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli za ushonaji na kujiongezea kipato.
"Hii cherahani ambayo ni ya kisasa tutaitunza ili iendelee kutunufaisha sisi wanakikundi,"amesena.
Mwisho.




0 Comments