TAKUKURU YASIMAMIA WAKULIMA 68 KUREJESHEWA MILIONI 54 ZA PAMBA.

Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu imefanikiwa kusaidia wakulima 68 wa zao la pamba wilayani Maswa kurejeshewa jumla ya Shilingi 54,442,755 walizokuwa wamezulimiwa na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) zao kwa kununuliwa pamba yao kwa mikopo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2026/2027.

Kupitia operesheni maalumu ya uchunguzi iliyofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, taasisi hiyo iliingilia kati suala hilo na kufuatilia madai ya wakulima hao hadi kufanikisha kurejeshwa kwa fedha zao.

Akitoa taarifa hiyo, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, Aron Gabriel Misanga, amesema hatua hiyo imewezesha wakulima 68 kupata fedha zao kabla ya kumalizika kwa msimu wa kilimo cha pamba wa mwaka huu.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Simiyu, Aron Gabriel Misanga, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za TAKUKURU katika kusimamia haki za wananchi, kudhibiti vitendo vya rushwa na ubadhirifu pamoja na kuhakikisha wakulima wanapata stahiki zao kutokana na mazao wanayozalisha.

Mafanikio hayo yanatoa ujumbe kwa wadau wote wa sekta ya pamba, hususan viongozi wa AMCOS na wanunuzi, kuzingatia uwazi, uadilifu na usimamizi mzuri wa fedha za wakulima ili kulinda maslahi yao na kuimarisha imani katika mfumo wa ununuzi wa mazao nchini.

Mwisho.



Post a Comment

0 Comments