
Na Mwandishi wetu, Busega,
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda amewataka madiwani na Watumishi wa Umma Wilayani Busega kuzingatia maadili, nidhamu, upendo na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya kuwahudumia Wananchi.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi hao katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, katika ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu ya kutembelea halmashauri.

Mtanda ameeleza kuwa maadili na nidhamu ni misingi muhimu inayopaswa kuzingatiwa na kila mtumishi wa umma ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia taratibu na sheria zilizowekwa.
Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kutambua dhamana waliyopewa na Serikali na kuitumia kwa manufaa ya wananchi, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kuathiri ufanisi wa utendaji kazi na imani ya wananchi kwa viongozi wao.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa upendo na kuheshimiana baina ya madiwani, watumishi wa umma na viongozi wengine katika maeneo yao ya kazi.
Ameeleza kuwa mazingira bora ya kazi hujengwa kwa kuzingatia mawasiliano mazuri, kusikilizana na kutatua changamoto kwa njia ya maelewano, jambo litakalosaidia kuimarisha mahusiano kazini na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Mtanda amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya madiwani na watumishi wa umma, akieleza kuwa makundi hayo yana majukumu yanayokamilishana katika kusimamia na kutekeleza mipango ya maendeleo. 
Amesisitiza kuwa ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja, kubadilishana mawazo na kuweka mbele maslahi ya wananchi badala ya tofauti binafsi, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na huduma za kijamii zinatolewa kwa ufanisi.
Mwisho.

0 Comments