Na Mwandishi wetu, Bariadi,
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amewataka wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wanaohitimu masomo na kuwasimamia kwa karibu ili kuhakikisha wanazingatia maadili mema na kuendelea na masomo kwa bidii hatua itakayowasaidia watoto hao kutimiza ndoto zao.
Ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 11 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kusekwa, iliyopo Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.
Mtanda amewasisitiza wazazi wajibu mkubwa wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kielimu na kijamii, hasa katika kipindi wanachomaliza hatua moja ya elimu na kujiandaa kuingia katika hatua nyingine ya maisha.
Amesema ushirikiano kati ya wazazi, walezi na watoto ni muhimu katika kuwajengea vijana mwelekeo mzuri wa maisha na kuwasaidia kufikia malengo yao.
Aidha, amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwabagua watoto wa kike katika upatikanaji wa fursa za elimu, akisisitiza kuwa watoto wote wanastahili kupata haki na nafasi sawa za kusoma bila kujali jinsia zao.
Amesema ni muhimu kwa wazazi kuwekeza katika elimu ya watoto wa kike na wa kiume kwa usawa ili kuwapa nafasi ya kutumia vipaji na uwezo wao katika kujiletea maendeleo na kulijenga taifa.
Katika hatua nyingine, Mtanda amewapongeza wanafunzi waliohitimu kwa kufikia hatua hiyo muhimu ya elimu, huku akiwahimiza kuendelea kusoma kwa bidii, kuwa na subira na kutokata tamaa wanapokutana na changamoto katika safari yao ya kielimu.
Mtanda pia amewataka Walimu na wazazi kutambua na kulea vipaji mbalimbali vya wanafunzi ili kuzalisha Taifa lenye watu wenye uwezo katika kulitumikia taifa katika sekta mbalimbali.
Amewakumbusha kuwa mafanikio yanahitaji nidhamu, kujituma, uvumilivu na matumizi sahihi ya muda katika kutimiza malengo waliyojiwekea.
Mahafali hayo ya 11 ya Shule ya Sekondari Kusekwa yamekuwa fursa ya kutambua juhudi za wanafunzi katika safari yao ya elimu, huku yakisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, wazazi na jamii kwa ujumla.
Ujumbe uliotolewa na Mtanda umeweka msisitizo katika malezi bora, usawa wa kijinsia katika elimu na wajibu wa kila mdau kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira yanayowawezesha kufikia ndoto zao.
Mwisho.







0 Comments