Na Mwandishi wetu.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa maono ya Dodoma kuwa Mji Mkuu wa Serikali yaliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.
Rais Dk. Samia ameyasema hayo leo Oktoba 30, 2026 jijini Dodoma kwenye uzinduzi wa majengo ya Mji wa Serikali yaliyoko Mtumba.
"Tarehe 24 Septemba 1973 Mkutano Mkuu wa 16 wa TANU uliamua Makao Makuu ya Tanzania yahamishiwe Dodoma. Tangu wakati huo, kila awamu ya uongozi imeendeleza azimio hilo, nami leo nimeungana na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Lourenço, kuzindua majengo ya ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma."
"Ninawashukuru Marais wote walionitangulia kwa kuendeleza maono ya Baba wa Taifa. Pia, nawapongeza viongozi, watendaji wa serikali na sekta binafsi, makandarasi na wananchi wote walioshiriki katika kutekeleza mradi huu. Kazi yenu ni ya thamani na itaenziwa katika historia ya nchi yetu."
" Mji huu uliojengwa kwa fedha za ndani umebuniwa kuwa kitovu cha shughuli za Serikali, huduma kwa wananchi, diplomasia na shughuli za kiuchumi na kijamii. Ni wajibu wetu kuhakikisha uwekezaji huu unaleta tija kwa kuwahudumia wananchi kwa heshima, weledi na ufanisi. Hata hivyo, huduma ziwafuate wananchi walipo kupitia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), badala ya kuwalazimu kufika Dodoma kuzifuata."
RAIS Dk. Samia amesisitiza kuwa Ili kuendeleza ustawi wa Mji huu na Makao Makuu kwa ujumla, nimetoa maelekezo yafuatayo:
1. Majengo, miundombinu na mazingira yatunzwe na kuwa safi wakati wote.
2. Mamlaka husika zisimamie kikamilifu utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Uendelezaji wa Jiji la Dodoma wa mwaka 2019–2039.
3. Wizara zinazohusika na huduma za kijamii zihakikishe huduma hizo zinapatikana kikamilifu.
4. Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji iendelee kuhamasisha na kuvutia uwekezaji ili kuunga mkono maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Mwisho









0 Comments