MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia, uliofanyika leo Oktoba 28, 2026.Na Mwandishi wetu.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuandaa mpango mkakati utakaowawezesha vijana na kampuni za Kitanzania kunufaika na fursa za ajira, zabuni na uwekezaji katika miradi ya mafuta na gesi asilia nchini.
Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 28, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini wa leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi - Wembere na Lindi- Mtwara, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuhakikisha Watanzania, hususan vijana na wanawake, wanapewa kipaumbele katika ajira, mafunzo, teknolojia na zabuni, huku kampuni za ndani zikiwezeshwa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Aidha, ameitaka Wizara ya Nishati kuimarisha mifumo ya tathmini, ufuatiliaji na usimamizi wa leseni hizo, sambamba na kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha, uwajibikaji na ongezeko la mapato ya Serikali kupitia kodi, mrabaha na mgao wa faida.
Ameielekeza TPDC kushirikiana na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, ujuzi na teknolojia ili kuongeza tija katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, huku akiwataka wadau kutanguliza uzalendo kwa Tafa, uadilifu, uchapa kazi na maslahi ya Taifa mbele.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, yanayozingatia uwazi, kutabirika kwa mifumo ya kisheria, ushindani wa haki na ulinzi wa maslahi ya Taifa.
Makamu wa Rais amesema, pamoja na lengo la kukuza pato la Taifa kufikia dola za Marekani trillioni 1 kama iliyoainishwa kwenye dira ya Taifa ya 2050. Matarajio mengine ya leseni hizo katika ugunduzi wa mafuta na gesi asilia ni ongezeko la mapato ya Serikali kupitia mrabaha, kodi na mgao wa faida.
Mwisho.





0 Comments