Na Samwel Mwanga, Maswa.
MKUU wa Polisi Wilaya ya Maswa, SSP, Samuel Onyango, amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo husika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wanaotuhumiwa.
Onyango amesema hayo Oktoba 14, 2026, katika Kijiji cha Mwanundi wilayani Maswa, mkoani Simiyu, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Ongea na Kamanda, inayolenga kuwaweka makamanda wa polisi karibu na wananchi kwa kusikiliza kero na malalamiko yao na kuyafanyia kazi.
Amesema mapambano dhidi ya uhalifu yanapaswa kuanzia katika ngazi ya familia na jamii, kwa kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kubaini na kudhibiti vitendo vya uhalifu mapema.
“Kila mmoja wetu hapa achukie vitendo vya uhalifu na wahalifu. Tuanze kudhibiti vitendo hivyo katika ngazi ya familia kwa kuwa wahalifu tunaishi nao katika jamii. Tusichukue sheria mkononi kwa kuwa nchi yetu inafuata utawala wa sheria,” amesema.
Onyango amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kutoa adhabu kwa watu wanaotuhumiwa kufanya uhalifu, akieleza kuwa mamlaka ya kutoa adhabu iko mahakamani.
Akizungumzia matarajio yao kuhusu kampeni hiyo, Joyce Iseme, mkazi wa Kijiji cha Mwanundi, amesema elimu ya sheria inapaswa kupewa kipaumbele ili kuwasaidia wananchi kutatua migogoro kwa kufuata taratibu zinazotambulika.
Amesema baadhi ya migogoro inaweza kuchochea chuki na visasi pale wahusika wanapokosa uelewa wa sheria na njia sahihi za kutafuta haki.
“Niwaombe viongozi wa kampeni hii kuweka msisitizo katika utoaji wa elimu ya sheria na kuhimiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo husika,” amesema.
Naye Francis Mafuja amesema kampeni hiyo haitakuwa na manufaa ya kutosha iwapo itajikita katika mikutano na utoaji wa elimu pekee bila kufuatilia malalamiko yanayotolewa na wananchi.
Amesema ni muhimu kero zinazowasilishwa katika mikutano hiyo zifanyiwe kazi ili wananchi wapate ufumbuzi wa matatizo yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.

“Utaratibu huu ni mzuri. Jambo la msingi ni kuhakikisha malalamiko yanayotolewa katika mikutano hii yanafanyiwa kazi ili ufumbuzi upatikane kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni bila mtu kuonewa,” amesema.
Kwa upande wake, James Khija amesema ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi utasaidia kubaini vitendo vya uhalifu mapema na kutoa taarifa kuhusu watu wanaotuhumiwa kuhusika na makosa ya jinai.
Amesema wananchi wanapaswa kutumia njia zinazotambuliwa kisheria kutatua migogoro badala ya kutumia nguvu, hali inayoweza kusababisha madhara na ukiukwaji wa haki.
Naye Mkuu wa Kamisheni ya Polisi Jamii Wilaya ya Maswa, ASP Michael Nchunga, amevitaka vikundi vya ulinzi vya kijamii kuzingatia sheria wakati wa kumkamata mtu anayetuhumiwa kufanya uhalifu.

Amesema ukamataji, upekuzi na uhoji wa watuhumiwa vinapaswa kufanyika kwa kuzingatia taratibu za kisheria na usalama wa wahusika ili kuepusha ukiukwaji wa haki.
“Tunachohitaji kutoka kwenu, vikundi vya ulinzi vilivyoko katika jamii, ni kuhakikisha ukamataji, upekuzi na uhoji wa mtuhumiwa yeyote vinafanyika kwa usalama na kwa kufuata taratibu, si vinginevyo. Hii itasaidia kupunguza vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi,” amesema.
Mwisho.




0 Comments