Na Costantine Mathias, SIMIYU.
WAANDISHI wa Habari Mkoa wa Simiyu wamepatiwa mafunzo yanayolenga kuwaongezea uelewa kuhusu usalama wa kidijitali, kujitambua pamoja na ulinzi na usalama wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
Mafunzo hayo yametolewa na Mary Kitoto kutoka Nyanza FM, ambaye amewajengea uwezo waandishi hao katika kutambua vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha usalama wao, taarifa zao, vifaa pamoja na mawasiliano yao ya kikazi katika mazingira ya sasa yenye matumizi makubwa ya teknolojia.
Akizungumza juzi wakati wa mafunzo hayo, katika ukumbi mdogo wa Nyanza Fm, Kitoto amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa makini katika matumizi ya vifaa na mifumo ya kidijitali, ikiwemo kulinda akaunti zao, taarifa muhimu na mawasiliano dhidi ya vitisho vinavyoweza kujitokeza mtandaoni.
Aidha, amesema kujitambua ni sehemu muhimu ya usalama wa mwandishi wa habari, kwa kuwa humsaidia kutambua uwezo na mipaka yake, kudhibiti hisia na kufanya maamuzi sahihi na yenye weledi hasa anapokabiliana na mazingira yenye changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake.
Katika eneo la ulinzi na usalama, waandishi wamefundishwa namna ya kutambua vihatarishi kabla na wakati wa kwenda kutekeleza kazi, kuchukua tahadhari stahiki na kuweka mikakati ya kujilinda dhidi ya vitisho vinavyoweza kuhatarisha usalama wao wa kimwili, kidijitali na kikazi.
Sitta Tuma, Mmliki wa STV ONLINE MEDIA, aliwataka waandishi wa habari kuchukua tahadhari wakati wakitekeleza majukumu yao ili kuendelea kuwa salama pamoja na vifaa vyao.
Katibu wa Simiyu Press Club (SMPC), Derick Milton aliwataka waandishi wa Habari kujiunga na klabu, kulipa ada pamoja na kuchangamkia fursa za mafunzo ili ziweze kuwaongezea ujuzi na kuleta ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya Habari.
Mafunzo hayo kwa waandishi wa habari Mkoa wa Simiyu yamefanyika baada ya Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kuwajengea uwezo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama, weledi na uwezo wa waandishi wa habari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mazingira ya uandishi wa habari.
Mwisho.

















































































0 Comments