VVYANDARUA 39,620 KUTOLEWA KWA WANAFUNZI KUDHIBITI MALARIA-SIMIYU.

‎Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

‎KUFUATIA kampeni ya Kupambana na Malaria, Mkoa wa Simiyu umepanga kugawa vyandarua 39,620 kwa wanafunzi wa shule za msingi wanaosoma darasa la tano na la sita.

‎Aidha, imeelezwa kuwa pamoja na jitihada za kukabiliana na Ugonjwa huo, Malaria imeshuka kutoka asilimia 11 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 4.3 mwaka 2025.

‎Akizungumza mwishoni mwa wiki jana kwenye Mkutano wa kampeni hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yudas Ndungile amesema kuwa Mkoa huo utatekeleza zoezi la Uwagaji wa vyandarua kwa wanafunzi walioko mashuleni katika Shule za serikali na binafsi.

‎Dk. Ndungile amesema kuwa Ugawaji na matumizi ya vyandarua hivyo ni njia mojawapo ya kujikinga na Malaria sababu Malaria ni mojawapo ya Magonjwa matano yanayouwa watu wengi duniani.

‎Ameeleza kuwa Ugawaji wa vyandarua ni njia mojawapo ya Kudhibiti Malaria huku akitaja njia zingine ni kumwaga dawa kwenye madimbwi pamoja na kutibu malaria.

‎Mwakilishi wa Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Kudhibiti Malaria, Gitaya Peter amesema kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha inatokomeza Ugonjwa wa Malaria ifikapo 2030.

‎Amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi saba katika bara la Afrika zenye kiwango kikubwa cha Ugonjwa wa Malaria hali inayosababisha vifo kwa watoto nchini.

‎"Vyandarua havina madhara yoyote, ni vyeupe, imara na havichaniki...Serikali imegharamia na vinatolewa bure, tuendelee kutoa Elimu ili vyandarua hivi vikatumike kama ilivyokusudiwa" amesema Gitaya.

‎Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo amewataka viongozi wote wanaohusika katika zoezi la Ugawaji wa vyandarua kutimiza wajibu wao ili zoezi hilo liweze kufanikiwa.

‎Kayombo amevitaka vyombo vya Ulinzi na usalama kuhakikisha wanasimamia zoezi hilo ili vyandarua visiweze kuibiwa wala kutumika isivyotakiwa.

‎"Sekta ya Afya na Elimu, mkashirikiane kuhakikisha zoezi linafanyika kwa asilimia 100, Uhamasishaji ngazi ya jamii uanze mapema... viongozi wa dini na nyumba za ibaada tukatoe Elimu Mskitini kupitia imani zetu, Vyandarua hivi havina athari yoyote" amesema Kayombo na kuongeza.

‎"Msitumie vyandarua hivi kufugia kuku au bustani, vyandarua havipunguzi nguvu, ni Kinga ya Malaria".

‎Mwisho.

‎

Post a Comment

0 Comments