Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Serikali inatambua changamoto ya kupanda kwa Bei ya saruji huku akiwahakikishia wananchi kuwa suala hilo la mfumuko wa Bei ya Saruji linashughulikiwa.
Amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesikia Kilio cha wananchi na ameelekeza wachukue hatua za haraka ili kidhibiti mfumuko wa bidhaa hiyo muhimu.
"Serikali ya CCM chini ya Rais Samia, itahakikisha inachukua hatua za haraka ili Bei ya saruji inakuwa himilivu ili kila Mtanzania aweze kuhimili kununua saruji hiyo...ndani ya wiki hii uamuzi utakuwa umefanyika ili tuweze kushughulikia tatizo hili na wananchi waendelee kujiletea Maendeleo" amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepiga Marufuku masuala ya kukamatwa bodaboda na kirikuu badala yake watumike utaratibu wa kufuata Sheria bila kubugudhi wananchi.
"Tusikamate Bodaboda badala yake walipe faini sababu wanafahamika kupitia Vitambulisho vya NIDA... nimeelekeza warudishiwe vitendea kazi vyao, maeneo mengine nimeona punda na mwenye mkokoteni wakikamatwa, msiwakamate, haya mengine ni ya kizamani, tumeweka Sheria msishikilie kitendea kazi cha mtu, mwacheni afanye kazi ili alipe faini." amesema.
Serikali kuimarisha sekta ya Afya.
Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali ya Rais Dk. Samia imeendelea kuimarisha huduma za Afya kwa kujenga vituo vya Afya, sahanati na hospitali za kisasa pamoja na kununua magari ya kubebe wagonja ili kuhakikisha huduma inaimarika.
"Serikali ya Dk. Samia imenunua ambulance za kisasa zenye ICU kila Mkoa kama za nchi za nje, inatokea mgonjwa huko anapelekwa hospital ya Rufaa wanaambiwa wakachangie Mafuta,
tunataka kuhararisha uzembe...mgonjwa mahututi anayepelekwa kwenye hospitali ya Rufaa asiombwe Mafuta na endapo wananchi mkimwona mtumishi huo mwangalie vizuri aliyewaomba Mafuta asihamishiwe bali afukuzwe kazi, Waziri fukuza huyo mtu sababu miongozo iko wazi".
Ameongeza kuwa Rais Dk. Samia amejenga hospitali na amepeleka Bajeti ya dawa, vitendanishi lakini wenye taarifa wanatajiwa utoshelevu 90%, na kwamba hakuna Mkoa usio na utoshelevu, wakati huo mgonjwa anaambiwa akanunue dawa mtaani.
Aelekeza Usanifu wa Barabara.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa ameelekeza kufanyika usanifu wa ujenzi wa Barabara ya Sibiti, Meatu, Mwandoya, Lagangabilili mpaka Bariadi ili waweze kufikia hatua za ujenzi.
"tumefanya vikao vitatu vitakavyofungua Barabara hii ya Sibiti, Meatu, Itilima, mpaka Bariadi na nimeelekeza wafanye usanifu ili iweze kufikia hatua za kuanza ujenzi...Nimelekeeza wafanye usanifu ili tufikie hatua za ujenzi, lakini pia serikali ya CCM imebadili utaratibu na Sheria ambapo sasa fedha za Barabara zinaenda kwenye Mfuko wa Barabara na siyo Wizara ya fedha, za TARURA, za maji, za Umeme zinakwenda Mfuko husika."
Ameeleza kuwa wataendelea kuepeleka fedha moja kwa moja, huku akiwatoa hofu wananchi ambapo wataweka kipaumbele kwenye Barabara hiyo muhimu ili kufungua Uchumi wa wananchi.
Sambamba na hayo, Waziri Mkuu amempongeza Dk. samia, kwa kutoa kiasi cha shilingi Trioni 1.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo katika Mkoa wa Simiyu.
Amesema kuwa kiasi cha shilingi Bil. 302 zimekwenda kwenye Miradi ya Umeme ambapo hadi sasa vijiji vyote vya Mkoa huo vimepata umeme, Shilingi Bil. 203 kwa ajili ya Barabara, Shilingi Bil. 91 kwa ajili ya Maji, Shilingi Bili. 138 kwa ajili ya sekta ya Elimu na shilingi Bil. 7.5 kwa ajili ya Afya.
Awali Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Silanga ameipongeza serikali kwa kutoa shilingi Bil. 12 kwa ajili ya sekta ya Afya ambapo wamejenga zahanati zaidi ya 15 na vituo vya Afya viwili na hospitali ya wilaya.
"Tumepokea shilingi Bil 17 za Elimu, ambapo tumejenga Sekondari 12, Shule za msingi 26, wananchi wanataka Maendeleo watoto wao wasome kupata viongozi kama wewe...Wanataka kila Kijiji wawe na Sekondari, haya mambo yako kwenye ilani ya CCM, tumepokea takribani Bil 12. kwa ajili ya ujenzi wa Barabara, sekta ya Maji, serikali imeleta Bil 7, shilingi bil. 41 za kutekeleza miradi ya Umeme.
Mbunge huyo alisema wananchi wanalalamikia suala la ununuzi wa Pamba kupitia Mpango mmoja huku aliiomba serikali kuangalia upya suala la ununuzi wa Pamba ili walime na wauze wakiwa huru pia aliomba kuharakisha Fidia ya Wanyama pori ili wananchi wapate haki yao kwani watu 5042.
Mkuu wa Mkoa, Saidi Mtanda aliipongeza serikali kwa kutoa kiasi cha shilingi Trioni 1.45 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo Katika Mkoa wa Simiyu huku akihakikisha Mkoa huo utaendelea kuimarisha Ulinzi na Usalama.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed, alisema Mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya Pamba na Tembo ambapo wananchi wanataka ushindani wa kuuza pamba ili waweze kupata na kuchagua soko au milango mingi ya kuuzia Pamba.
Mwisho.











0 Comments