Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Dulungwa wilaya ya Maswa.Picha na Samwel Mwanga.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
MBUNGE wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki, amewataka wananchi wa kijiji cha Dulungwa, Kata ya Kadoto wilaya ya Maswa, kushikamana katika shughuli za maendeleo badala ya kuwekeana vikwazo.
Akizungumza Septemba 17, 2026, katika mkutano wa hadhara kijijini hapo amesema kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakipinga matumizi ya kisima kirefu kama chanzo cha mradi wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa).
Amesema hali hiyo imesababisha kuwepo kwa makundi yanayopingana, jambo linalochelewesha utekelezaji wa mradi.
“Tukumbatie maendeleo na siyo kupingana. Kwa sasa kwa pamoja tuzungumze lugha ya maendeleo, ndiyo maana mimi nikija hapa sizungumzii masuala ya siasa,” amesema.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha (wa pili kushoto) akitoa maelezo kwenye kisima cha maji ambacho watakiendeleza kama chanzo cha maji.Picha na Samwel Mwanga.Amesema serikali imechukua hatua ya kutumia kisima hicho baada ya kubainika kuwa kina maji ya kutosha, hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo.
Kwa upande wake, Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha, amesema kuwa walifanya jitihada za kutafuta chanzo kingine lakini hawakufanikiwa, hivyo wakaamua kutumia kisima hicho.
Amesema pampu ya mkono iliyopo katika kisima hicho itaendelezwa kwa kufungwa mfumo wa nishati ya umeme wa jua utakaosukuma maji kwenda kwenye tenki lenye ujazo wa lita 10,000.
“Katika kisima hiki cha pampu ya mkono tutakiendeleza kwa kuweka nishati ya umeme wa jua ili uweze kuvuta maji kwenda kwenye tenki lenye ujazo wa lita 10,000 ili liweze kusambaza maji kutoka katika kitongoji cha Nyashishi hadi eneo lote la kijiji cha Dulungwa,” amesema.
Amesema mradi huo pia utakuwa na eneo maalumu kwa ajili ya mifugo, huku Sh120 milioni zikitumika katika mpango huo wa muda mfupi.
“Huu ni mpango wa muda mfupi kuhakikisha kijiji hiki kinapata maji na kiasi cha Sh120 milioni kitatumika katika mradi huu na ukikamilika mwananchi atapata huduma ya maji kwa gharama ya Sh45 kwa ndoo moja ya lita 20,” amesema.
Amesema kuwa mgogoro kuhusu matumizi ya kisima hicho umesababisha mradi kusimama na kuchelewesha utekelezaji wake.
Wananchi wanavyosema.
Magreth Kanogu, mkazi wa Dulungwa, amesema wananchi wanahitaji mradi huo ukamilike ili kuondokana na changamoto wanayokutana nayo katika maisha ya kila siku.
“Tunaiomba Serikali kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa sababu bado tunapata shida kubwa katika upatikanaji wa huduma hii,” amesema.
Gogadi Lutema amesema kuchelewa kwa mradi huo kunaathiri shughuli za uzalishaji, hasa kwa wanawake wanaotumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo.
“Wanawake wanatumia muda mwingi kutafuta maji, jambo linalowafanya wakose muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” amesema.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Dulungwa wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mkutano wa mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki.Khija Malando amesema wananchi wanapaswa kuweka mbele maslahi ya kijiji na kuepuka mambo yanayoweza kuzuia utekelezaji wa mradi.
“Watu wanaokwamisha mradi huu wanaangalia zaidi maslahi yao binafsi. Tunapaswa kuangalia manufaa yake kwa wananchi wote wa kijiji,” amesema.
Mwisho.





0 Comments