MASHIMBA NDAKI AKABIDHI MADAWATI 161 KUPUNGUZA WANAFUNZI KUKAA CHINI.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa (kushoto) akimkabidhi Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki dawati ambalo amelitengeneza kupitia fedha zake binafsi.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki, amekabidhi madawati 161 yenye thamani ya Sh10 milioni kwa shule za msingi katika jimbo hilo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza tatizo la upungufu wa madawati unaowalazimu baadhi ya wanafunzi kukaa chini wakati wa masomo.

Madawati hayo yamegawanywa katika shule sita za msingi, huku kila dawati likigharimu Sh. 62,100. 

Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki akizungumza wakati wa halfa ya kukabidhi madawati 161 ya shule za msingi.

Madawati 12 yametengenezwa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na kuelekezwa katika Shule ya Msingi Jija B ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za mbunge huo.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Septemba 30, 2026 katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Binza, mjini Maswa, na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, wakuu wa divisheni na vitengo pamoja na Waratibu Elimu Kata.

Sehemu ya madawati 161 yaliyotengenezwa na Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi,Mashimba Ndaki kwa ajili ya shule za msingi katika jimbo hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Ndaki amesema mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali na uongozi wa wilaya ya Maswa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Madawati haya ni sehemu ya mchango wetu katika kuunga mkono juhudi zinazofanyika wilayani Maswa. Tunataka watoto wasome katika mazingira mazuri na wasilazimike kukaa chini wakati wa masomo,” amesema.

Dkt Naano amesema mpango wa kukabiliana na upungufu wa madawati ulianzishwa baada ya kubaini kuwa wilaya hiyo ina upungufu wa zaidi ya madawati 2,000, hivyo serikali kuamua kuhusisha wananchi na wadau mbalimbali katika kutafuta suluhisho.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dkt Vicent Naano Anney akizungumza wakati wa halfa ya kukabidhi madawati 161 ya shule za msingi.

Amesema ushiriki wa Mbunge Ndaki na watumishi wa serikali katika mpango huo ni sehemu ya mwitikio unaohitajika ili kupunguza changamoto hiyo.

“Tulibaini kuwa wilaya yetu ina upungufu wa madawati na baadhi ya wanafunzi wakiwa darasani wanakaa chini ndiyo maana tukaona ni lazima tuanzishe mpango wa pamoja unaowahusisha wananchi, serikali na wadau wengine ili kuhakikisha tatizo hili linaondoka,” amesema

Amesema hatua hiyo inapaswa kuendelea kwa kushirikisha wadau wengine ili kuhakikisha shule zote zenye upungufu zinapatiwa madawati.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema watumishi wa halmashauri hiyo kupitia divisheni na vitengo mbalimbali wameamua kuwa sehemu ya mpango huo kwa kushiriki katika utengenezaji wa madawati.

“Watumishi wa halmashauri tumeona ni muhimu kuwa sehemu ya mpango huu. Madawati 12 tuliyoyatengeneza ni mwanzo wa mchango wetu katika kupunguza tatizo hili,” amesema.

Wananchi nao wameunga mkono mpango huo, wakisema upatikanaji wa madawati utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kupunguza changamoto ya kukaa chini.

Silivester Lugembe ni mkazi wa mtaa wa  Unyanyembe mjini Maswa mkazi amesema kuwa mpango huo una umuhimu kwa wanafunzi kwa kuwa unalenga kutatua changamoto inayowakabili wakati wa masomo.

Thomas Jinasa mkazi wa Majebele mjini Maswa amesema kuwa madawati hayo yatawasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora zaidi.

Madawati hayo yanatarajiwa kuongeza nafasi za kukaa kwa wanafunzi katika shule zilizonufaika na kuunga mkono mpango wa Wilaya ya Maswa wa kupunguza upungufu wa madawati katika shule za msingi.

Mwisho.






Post a Comment

0 Comments