JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LAWAPATIA MAFUNZO REDCROSS-SIMIYU.



Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto kwa Wanachama na Voluntia wa shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) mkoani humo.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo tarehe 11 Septemba, 2026, eneo zilipo Ofisi za jeshi hilo mkoani humo, katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ni moja ya mikakati ya kukabiliana na majanga, ikiwamo wakati wa mvua kubwa za El-Nino zinazotabiriwa kutokea mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika mafunzo hayo endelevu, elimu iliyotolewa kwa Wanachama na Voluntia wa Red Cross pamoja na askari wa jeshi hilo la uokoaji, ni pamoja na aina mbalimbali ya moto ukiwamo moto wa mimea.



Aina nyingine ni moto wa vyuma, gesi, vimiminika vinavyowaka moto, ambapo wahusika wamefundishwa mbinu na namna ya kuidhibiti bila kuleta athari kwa raia na mali zao.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustin Mtitu, amesifu ushirikiano wa jeshi hilo na Red Cross mkoani hapa.

Amesema pande zote zinaendelea kuimarisha elimu ya kukabiliana na majanga, pamoja na utoaji wa huduma ya kwanza kwa jamii zenye uhitaji wakati na mahala popote, kabla, wakati na baada ya mvua za el-nino.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Red Cross Mkoa wa Simiyu, Sitta Tumma, amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu ya kuisaidia jamii wakati wa majanga.

Amesema katika kipindi cha kuelekea kwenye mvua za El-Nino, Red Cross Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, hawatasalia nyuma katika uimarishwaji wa elimu ya kukabiliana na majanga na huduma ya kwanza kwa jamii yote.

"Ni muhimu kujiandaa vizuri leo, ili kesho ufanye vizuri zaidi. Hivyo, mafunzo haya kwetu ni kielelezo cha mafanikio katika kuihudumia jamii kwa weledi," amesema Sitta Tumma, Mwenyekiti wa Red Cross Mkoa wa Simiyu.

Mwisho.











Post a Comment

0 Comments