DC BARIADI ATOA ONYO NGOs ZINAZOKIUKA MAADILI YA KITANZANIA.

Mkuu wa wilaya hiyo, Simon Simalenga akizungumza kwenye jukwaa la Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).

Na Mwandishi wetu.

MASHIRIKA  yasiyo ya kiserikali (NGOs), wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, yametakiwa kutekeleza Majukumu Yao katika Jamii kwa kuzingatia maadili huku mashirika hayo yakionywa kutojihusisha na miradi au vitendo vinavyokiuka mila, desturi, na maadili halisi ya Kitanzania.

Akizungumza wakati akifungua jukwaa la Mwaka wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Wilaya ya Bariadi kwa Mwaka 2026, Mkuu  wa wilaya hiyo, Simon Simalenga amesema serikali inatambua kazi kubwa zinazofanywa na mashirika hayo yasiyo ya kiserikali hivyo yanapaswa kufanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria ya kuanzishwa kwake.

“Mashirika  yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini yanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, na kulinda mila, desturi, na maadili mema ya jamii ya Kitanzania”Amesema Simalenga.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameyataka Mashirika hayo kufanya kazi kwa kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii ili waweze kutambua kazi au majukumu wanayofanya kipindi wakitekeleza miradi yao ngazi ya jamii badala ya kutekeleza majukumu yao wakiwa pekee yao.

Wilaya ya Baridi ina jumla ya mashirika (35) yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yanatekeleza miradi mbalimbali katika sekta za Elimu, Afya, Mazingira na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Jukwaa hilo limefanyika leo 28 Septemba 2026 katika Ukumbi wa Mikutano ya Ofisi  ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi na kuhudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Bariadi.

MWISHO.














Post a Comment

0 Comments