DC ANNEY AKEMEA MPASUKO MAMLAKA YA MJI MDOGO MASWA.

 

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Anney akizungumza katika kikao cha baraza la mamlaka ya mji mdogo wa Maswa. Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga, Maswa.

MKUU wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Anney, ameitaka Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria na miongozo, badala ya kujikita katika migogoro ya ndani.

Akizungumza Septemba 9, 2026 katika kikao cha baraza la mamlaka hiyo, amesema hatavumilia mpasuko unaodaiwa kuwagawa wajumbe katika makundi mawili.

Amesema licha ya mamlaka hiyo kuanzishwa zaidi ya miaka 15 iliyopita, bado haijafikia vigezo vya kupandishwa hadhi kuwa halmashauri ya mji, akitaja ufanisi mdogo kuwa miongoni mwa sababu.

“Huu mpasuko hauna tija kwa kuwa unaondoa umoja na mshikamano. Ninyi nyote ni viongozi katika maeneo yenu, ni lazima mjitambue,” amesema.

Amesema hali hiyo imekuwa ikikwamisha baadhi ya shughuli za maendeleo, ikiwamo utengenezaji wa madawati na utoaji wa chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi.

“Tufanye kazi kama timu moja. Sitarajii kuwa na baraza la majungu. Ningekuwa na mamlaka ya mwisho, ningeshauri kuvunjwa kwa mamlaka hii ili turudi kwenye vijiji,” amesema.

Pia amekemea baadhi ya wajumbe kumshambulia kwa maneno Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, akiwataka viongozi hao kuheshimu majukumu yao.


“Una hoja chanya, iwasilishe vizuri, si hadi jasho likutoke,” amesema.

Mjumbe wa mamlaka hiyo, Agustino Kabuta, amesema tofauti hizo zinapaswa kumalizwa ili waweze kuhudumia wananchi.

“Ni lazima tuheshimiane. Twendeni kwa umoja, kwa sababu tukiwa vipande vipande hatutaweza kufikia malengo,” amesema.

Mjumbe mwingine, Antony Peter, amesema baadhi ya changamoto zinatokana na wajumbe kutopatiwa mafunzo ya majukumu yao kabla ya kuanza kazi, hali inayoweza kusababisha mwingiliano wa majukumu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mamlaka hiyo, Caroline Shayo, amesema kutokuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya mamlaka hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ni chanzo cha migogoro ya mara kwa mara.

Wananchi wanena.

Jesca Magare amesema wananchi wanahitaji viongozi wanaojikita katika kutatua changamoto za huduma badala ya migogoro.

“Wananchi hatuna shida na nani yuko upande gani. Tunachotaka ni viongozi kukaa pamoja na kutatua matatizo yetu,” amesema.

Baadhi ya wajumbe wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa wakiwa kwenye kikao cha baraza la Mamlaka hiyo.Picha na Samwel Mwanga

Samson Mathias amesema muda mrefu wa mamlaka hiyo unapaswa kuonekana katika matokeo ya maendeleo.

“Viongozi wakigombana wananchi ndio tunaumia. Tofauti zao ziwekwe pembeni na wafanye kazi,” amesema.

Naye Ramadhan Said amesema migogoro kati ya mamlaka na halmashauri inapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo na kuheshimiana.

“Kama kuna tatizo, watafute utaratibu wa kulimaliza kwa sababu wananchi ndio wanaotegemea huduma zao,” amesema.

CCM yataka maagizo yazingatiwe.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa, Mwl Onesmo Makota, amesema wajumbe wa mamlaka hiyo wametokana na chama hicho, hivyo wanapaswa kutekeleza maagizo yanayotolewa kwa lengo la kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa,Onesmo Makota akizungunza katika kikao cha baraza la Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa.Picha na Samwel Mwanga

Amesema viongozi hao wanapaswa kuweka tofauti zao pembeni na kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

“Wajumbe hawa wametokana na CCM, hivyo wanapaswa kutimiza maagizo yote yanayotolewa kwa lengo la kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo, si vinginevyo,” amesema.

MWISHO.


Agustino Kabuta ambaye ni mjumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo wa Maswa akitoa mchango wake wa mawazo katika kikao.Picha na Samwel Mwanga.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa,Caroline Shayo akiongoza kikao cha baraza la mamlaka hiyo.Picha na Samwel Mwanga

Post a Comment

0 Comments