SERIKALI: NANENANE IBADILI KILIMO CHA MAZOEA KUWA BIASHARA.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Leonard Akwilapo, (wa nne kushoto), akiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu wakikagua vizimba vya kufugia samaki katika Viwanja vya maonyesho ya wakulima na Wafugaji Vya nanenane Nyakabindi.

Na Samwel Mwanga, Bariadi.

SERIKALI imewahimiza Wakulima, Wafugaji na Wadau wa sekta ya kilimo nchini kutumia maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kujifunza teknolojia na mbinu za kisasa zitakazowasaidia kuachana na kilimo cha mazoea na kuelekea kwenye kilimo biashara.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Leonard Akwilapo, amesema hayo jana Agosti 8, 2026, katika viwanja vya Nanenane vya Nyakabindi mkoani Simiyu, mara baada ya kutembelea vipando na mabanda ya maonesho ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Amesema maonesho hayo yanapaswa kuwa zaidi ya sehemu ya wananchi kuja kutazama bidhaa na teknolojia, bali yawe fursa ya kupata elimu itakayowasaidia kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda na vipando vya JKT katika viwanja vya Nanenane vya Nyakabindi mkoani Simiyu. Picha na Samwel Mwanga.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda na vipando vya JKT katika viwanja vya Nanenane vya Nyakabindi mkoani Simiyu.Picha na Samwel Mwanga

“Maonesho haya yatoe fursa ya kuwabadilisha wakulima, wafugaji na wavuvi ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija,” amesema.

Dkt Akwilapo amesema maonesho ya mwaka huu yameboreshwa kwa kiwango kikubwa kutokana na wananchi kupata fursa ya kujionea teknolojia za kisasa zinazotumika katika sekta ya kilimo, huku wakiwa na nafasi ya kupata mbegu bora na elimu kuhusu kanuni za kilimo bora.

Amesema elimu inayotolewa na wataalamu katika maeneo mbalimbali ya maonesho, ikiwamo JKT, inapaswa kutumika na wananchi katika kuboresha shughuli zao wanaporudi kwenye maeneo yao.

Mfugaji wa ng'ombe,Yusuph Opi (mwenye fulana rangi ya kijani) wa halmashauri ya wilaya ya Maswa akitoa maelezo juu ya ufugaji wa ng'ombe wa kisasa kwa wananchi waliotembelea banda hilo katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.Picha na Samwel Mwanga

"Elimu ya kilimo, mifugo na uvuvi inayotolewa hapa kwenye viwanja vya Nyakabindi, hasa katika haya maeneo ya JKT, kwa kweli ni lazima iwabadilishe wananchi wanaofanya shughuli hizo. Maana wataalamu hawa wamejipanga vizuri kuonyesha wanachokifanya ili kuleta tija,” amesema.

Amesema mabadiliko ya teknolojia katika kilimo yanapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya fikra kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili shughuli hizo ziwe chanzo cha kipato na ajira badala ya kuendelea kufanyika kwa mazoea.

Kwa mujibu wa Dkt. Akwilapo, matumizi ya teknolojia, mbegu bora, ufuatiliaji wa masoko na kuzingatia ushauri wa wataalamu ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza uzalishaji na kumwezesha mkulima kupata faida.

Wananchi: Tunahitaji elimu itakayotekelezeka.

Mkulima kutoka Simiyu, Juma Matondo amesema moja ya faida kubwa ya maonesho hayo ni kupata fursa ya kuona kwa vitendo mbinu mpya za kilimo ambazo awali alikuwa akizisikia bila kuziona.

Amesema elimu inayotolewa kwenye maonesho imemsaidia kuelewa kuwa kuongeza uzalishaji hakutegemei ukubwa wa shamba pekee, bali pia matumizi ya mbegu bora, maandalizi sahihi ya shamba na kuzingatia wakati unaofaa wa kupanda.

“Tumekuwa tukilima kwa mazoea kwa muda mrefu. Unapokuja hapa unaona mbinu ambazo zinaweza kukufanya uzalishe zaidi katika eneo lilelile. Sasa changamoto ni kuhakikisha elimu hii tunaenda kuifanyia kazi mashambani,” amesema.

Kwa upande wake, mfugaji Musa Magesa kutoka mkoa wa Mara  amesema maonesho hayo yamemsaidia kutambua umuhimu wa kubadili mfumo wa ufugaji wa jadi na kutumia mbinu zinazolenga kuongeza tija na kipato.

Amesema wafugaji wanahitaji kuendelea kupewa elimu kuhusu ufugaji bora, lishe ya mifugo, uzalishaji wa mifugo yenye ubora na matumizi sahihi ya ardhi ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

“Ufugaji wa sasa hauwezi kuwa wa kuachia mifugo itafute malisho yenyewe bila mipango. Hapa tumeona mbinu za kisasa ambazo zinaweza kutusaidia kuongeza uzalishaji. Tukizitumia, mfugaji anaweza kuona tofauti kwenye kipato chake,” amesema.

Martine Nsongoma (kulia)Mtafiti na Mkaguzi wa mbegu (TOSCI) Kanda ya Ziwa akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea banda la TOSCI katika viwanja vya Nanenane vya Nyakabindi mkoani Simiyu.Picha na Samwel Mwanga

Naye Hassan Juma, mvuvi kutoka eneo la Ziwa Victoria wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu, amesema sekta ya uvuvi pia inahitaji kupewa kipaumbele katika maonesho kama hayo kwa kuwa teknolojia na elimu vinaweza kuwasaidia wavuvi kuongeza tija huku wakizingatia uhifadhi wa rasilimali za uvuvi.

Amesema wavuvi wanahitaji elimu ya mara kwa mara kuhusu matumizi ya zana sahihi za uvuvi, uhifadhi wa mazingira ya maji na namna ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.

“Tunachohitaji siyo tu kuvua samaki wengi, bali kujua namna ya kufanya uvuvi wenye tija na unaolinda rasilimali hii...Elimu tunayopata hapa ikifika kwa wavuvi wengi inaweza kubadilisha maisha yao,” amesema.

Maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu, yamewakutanisha wakulima, wafugaji, wavuvi, wataalamu, taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali wa kilimo.

Kaulimbiu ya Nanenane mwaka huu ni “Tambua soko, zalisha kwa tija, kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Mwisho.






Post a Comment

0 Comments