POLISI JAMII YAPUNGUZA VITENDO VYA UHALIFU.

Mwanafunzi Veronica Ally (aliyekati) wa shule ya msingi Shanwa akitoa shukrani kwa jeshi la polisi mara baada ya kuwatembelea shuleni hapo.Picha na Samwel Mwanga

Samwel Mwanga, Maswa.

KAMISHENI  ya Polisi Jamii mkoani Simiyu imesema uwepo wa Polisi Jamii umesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya uhalifu katika jamii, kutokana na matumizi ya elimu na ushirikishwaji wa wananchi katika kupambana na uhalifu.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Asiago Ochieng amesema hayo  leo Agosti 31,2026 wakati wa shughuli za kijamii zilizofanyika katika Shule ya Msingi Shanwa, wilayani Maswa.

Amesema kupitia Kamisheni hiyo, Jeshi la Polisi linatumia njia ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya usalama, huku likibaini changamoto zinazowakabili na kuziwasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

Mkuu wa Polisi Jamii mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi,Asiago Ochieng akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Shanwa (hawako pichani).Picha na Samwel Mwanga.

“Hakuna sababu kwa jamii kuliogopa Jeshi la Polisi. Wafike na kutupatia taarifa za uhalifu na wahalifu ambao nao ni sehemu ya jamii,” amesema.

Amesema Jeshi la Polisi ni sehemu ya jamii na linahitaji ushirikiano wa wananchi ili kuhakikisha usalama unakuwepo katika maeneo wanayoishi.

“Hatutaki jamii ituogope kwa sababu nasi ni sehemu ya jamii. Tunaishi ndani ya jamii na mahitaji yetu tunayapata kutoka katika jamii,” amesema.

Amesisitiza wananchi kutoa taarifa za kijamii na kiusalama kwa Polisi, akisema taarifa hizo ni muhimu katika kubaini na kuzuia uhalifu kabla haujatokea au kuleta madhara makubwa.

Mkuu wa Polisi Jamii mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Asiago Ochieng (kushoto) akiwa na mwanafunzi Mbuke Samwel (kulia) ambaye anaishi katika mazingira magumu ambaye amepatiwa msaada wa kipekee wa vifaa vya shule na jeshi hilo na kuhaidiwa kusomeshwa zaidi.Picha na Samwel Mwanga.

Katika shughuli hiyo, Kamisheni ya Polisi Jamii ilitembelea Shule ya Msingi Shanwa, ambayo ilianzishwa mwaka 1928, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii.

Shule hiyo pia ina historia ya kuwa miongoni mwa maeneo yaliyotoa viongozi mbalimbali, akiwemo Kamishna wa Polisi (CP) Mstaafu Faustine Shilogile, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Polisi Jamii.

Shilogile alisoma katika shule hiyo na kumaliza darasa la saba mwaka 1979. Ziara hiyo pia ilikuwa sehemu ya kumuenzi Shilogile ambaye mwaka 2024 alipanda mti katika eneo la shule hiyo.

Mbali na kupanda miti, Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii lilitoa vifaa mbalimbali vya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule hiyo, vikiwemo madaftari na kalamu.

Aidha, Jeshi hilo limechukua jukumu la kumsomesha mwanafunzi Mbuke Samwel, anayesoma darasa la saba katika shule hiyo na anayeishi katika mazingira magumu, hatua inayolenga kumwezesha kuendelea na masomo atakapohitimu elimu ya msingi na kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Mwanafunzi huyo amepata msaada huo wakati ambao yuko katika hatua muhimu ya kumaliza elimu ya msingi, huku Jeshi la Polisi likilenga kuhakikisha changamoto za kifedha hazimzuii kuendelea na elimu ya sekondari.

Ochieng amesema shughuli hizo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii inayolenga kuwaleta karibu zaidi askari na wananchi, kujenga uaminifu na kuongeza ushirikiano katika masuala ya usalama na maendeleo ya jamii.

Amesema ushirikiano huo unapaswa kuendelea kwa wananchi kutoa taarifa kwa wakati kuhusu vitendo vya uhalifu, watu wanaotuhumiwa kujihusisha na uhalifu pamoja na changamoto nyingine zinazohitaji hatua za mamlaka.

Kwa mujibu wa Ochieng, Polisi Jamii itaendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni pamoja na elimu, uhifadhi wa mazingira na kusaidia makundi yenye mahitaji, huku ikisisitiza kuwa usalama wa jamii ni jukumu linalohitaji ushirikiano wa pande zote.

Akizungumza kuhusu msaada huo, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo, Veronica Ally, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwatembelea na kushiriki shughuli za uhifadhi wa mazingira shuleni hapo.

Amesema upandaji wa miti uliofanywa na jeshi hilo utasaidia kulinda mazingira ya shule, huku akiwaahidi kwa niaba ya wanafunzi wenzake kuitunza miti hiyo ili ikue na kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.

“Tunawashukuru Jeshi la Polisi kwa kututembelea na kupanda miti katika shule yetu. Tutaendelea kuitunza ili ilinde mazingira yetu,” amesema Veronica.

Naye Shija Malimi, mwanafunzi wa shule hiyo, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwapatia vifaa vya kujifunzia, akisema msaada huo umewasaidia wanafunzi ambao wazazi au walezi wao hawana uwezo wa kutosha wa kuwanunulia mahitaji ya shule.

Ameziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo wa Jeshi la Polisi kwa kutoa msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji, akisema hatua hiyo inaweza kuwasaidia kuendelea na masomo bila kukatishwa na changamoto  za ukosefu wa vifaa.

“Tunawashukuru kwa kutupatia vifaa vya kujifunzia. Tunaomba taasisi nyingine zije kuiga mfano huu kwa sababu kuna wanafunzi ambao wazazi au walezi wao hawana uwezo wa kuwapatia vifaa vya shule,” amesema.

Mwisho.







Post a Comment

0 Comments