MASWA DC YAICHAPA IRINGA DC 2-0 SHIMISEMITA MBEYA.



Timu ya soka ya Halmashauri ya wilaya ya Maswa(Maswa Dc)iliyoifunga timu ya Halmashauri ya wilaya ya Iringa kwa magoli 2-0 katika mashindano ya SHIMISEMITA yanayofanyika jijini Mbeya.Picha na Samwel Mwanga.


Na Samwel Mwanga,Mbeya.

MASWA DC imeendeleza wimbi la ushindi katika mashindano ya SHIMISEMITA 2026 yanayoendelea jijini Mbeya, baada ya kuichapa Iringa DC mabao 2-0 katika mchezo wa soka uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga.

Maswa DC ilionyesha kiwango kizuri cha soka, huku ikitawala sehemu kubwa ya mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, ingawa ililazimika kusubiri hadi kipindi cha pili kupata mabao hayo mawili.

Mshambuliaji Sunday Amani ndiye aliyeifungulia Maswa DC ukurasa wa mabao, kabla ya Ninde Liganga maarufu kwa jina la Chico kuongeza bao la pili na kuhitimisha ushindi wa timu hiyo.

Licha ya ushindi huo wa mabao 2-0, Maswa DC imebaki na jambo la kujilaumu baada ya kushindwa kutumia ipasavyo nafasi kadhaa ilizotengeneza, hasa katika eneo la mwisho ambako umakini mdogo katika kumalizia ulifanya baadhi ya nafasi nzuri zipotee.

Mashambulizi ya Maswa DC yaliendelea kuonekana kuwa na tishio kwa safu ya ulinzi ya Iringa DC, lakini ukosefu wa umakini katika mipira ya mwisho uliifanya timu hiyo kushindwa kuongeza idadi ya mabao licha ya kupata nafasi za kutosha.

Ushindi huo unaipa Maswa DC morali zaidi katika safari yake ya kuwania kufanya vizuri kwenye SHIMISEMITA 2026, huku macho ya mashabiki yakielekezwa kwenye michezo inayofuata.

Kwa upande wa Iringa DC, kipigo hicho kimeifanya timu hiyo kukutana na changamoto kubwa katika harakati zake za kuendelea kufanya vizuri katika mashindano hayo yanayoshirikisha halmashauri mbalimbali nchini.

Mwisho.








Post a Comment

0 Comments