Mifuko 200 ya Saruji pamoja na Mabati 212 yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew kwa lengo la kuchochea Maendeleo kata ya Bariadi.Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew amekabidhi jumla ya mifuko ya Saruji 200 pamoja na Mabati 212 kwa ajili ya kuchochea ujenzi wa miradi ya Maendeleo katika sekta za Utawala, Elimu Msingi na Sekondari kwenye Kata ya Bariadi Mjini Bariadi.
Mhandisi Kundo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, amekabidhi vifaa hivyo akiwa kwenye ziara yake ya Kata kwa Kata yenye lengo la kuwashukuru wananchi, kutatua kero zao pamoja na kuwasilisha Mpango wa Bajeti ya Serikali 2026/2027.
Katika ziara hiyo, Mbunge huyo amekabidhi bati 100 na mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Bariadi, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi pia amekabidhi bati 54 kwa ajili ya kukarabati darasa moja la Shule ya Msingi Kidinda lililoungua moto ili kurejesha mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Vilevile, Mbunge Kundo amekabidhi bati 58 na mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kukamilisha chumba darasa la kompyuta katika Shule ya Sekondari Kidinda, hatua itakayochochea maendeleo ya TEHAMA na kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni.
Katika ziara hiyo, Mhandis Kundo aliambatana na wataalamu wa serikali kutoka kila idara ikiwemo sekta ya Elimu, Afya, Maji, Umeme, Barabara, Ardhi, Kilimo, Mifugo, Biashara na zinginezo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Akiwa kwenye Mkutano huo, Mhandisi Kundo amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo imejikita kutatua kero za wananchi.
Mwisho.






0 Comments