DC MASWA AWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI MVUA ZA EL-NINO.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo.Picha na Samwel Mwanga

Samwel Mwanga, Maswa.

MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dkt. Vicent Anney, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazotarajiwa za El-Nino kwa kutunza chakula, kuimarisha makazi na kuhama kutoka maeneo ya mabondeni.

Akizungumza  Agosti 28, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Wilaya ya Maswa, amesema maandalizi ya  mapema ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.

Amesema taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu uwezekano wa mvua hizo kunyesha katika baadhi ya maeneo, ikiwamo mkoa wa Simiyu, zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na wananchi pamoja na viongozi katika ngazi zote.

Sehemu ya baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo.Picha na Samwel Mwanga

“Wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema, kuhakikisha wanatunza chakula, wanaimarisha nyumba zao na miundombinu inayowazunguka, na wale wanaoishi katika maeneo ya mabondeni waanze kutafuta maeneo salama kabla hali haijawa mbaya,” amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea kwa maafa ikiwamo uharibifu wa nyumba, upotevu wa mali na changamoto za upatikanaji wa chakula endapo mvua zitakuwa kubwa kuliko kawaida.

Dkt. Anney pia amewataka viongozi wa vijiji, mitaa na kata kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maeneo hatarishi na umuhimu wa kuchukua hatua za kinga kabla ya mvua kuanza kwa nguvu.

"Tahadhari hii si ya wananchi pekee, bali viongozi wa maeneo mbalimbali tunapaswa kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati na kuchukua hatua pale inapobainika kuna maeneo yenye hatari,amesema.

Amesema usalama wa maisha ya wananchi unapaswa kupewa kipaumbele, huku akiwataka wananchi kutopuuza taarifa na maelekezo yatakayotolewa na mamlaka husika kuhusu mwenendo wa mvua hizo.

Sehemu ya baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha baraza hilo.Picha na Samwel Mwanga

Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia wilaya hiyo kujiandaa mapema na kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa, ikiwa ni pamoja na mafuriko na uharibifu wa makazi na mali.

Slivester Lugembe ni mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa ni vizuri kwa kila familia kuangalia usalama wao.

“Tumepokea tahadhari hii vizuri. Cha muhimu sasa ni kila familia kuangalia usalama wa nyumba yake, chakula na mali zake. Hatupaswi kusubiri mvua zianze ndipo tuchukue hatua,” amesema.

Naye Edita John wa Malampaka amesema kuwa  taarifa hizo zinapaswa kufuatwa na hatua za haraka, hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni.

“Watu wanaoishi maeneo hatarishi wanahitaji kupewa elimu na kusaidiwa kutafuta maeneo salama. Mvua kubwa inaweza kuleta madhara makubwa ikiwa maandalizi hayatakuwa ya mapema,” amesema.

Kwa upande wake, Madeleke Jiloba mkazi wa kijiji cha Mwabayanda "M" amesema wananchi wanapaswa pia kuimarisha mifumo ya maji, kusafisha mitaro na kuondoa vitu vinavyoweza kuzuia maji kupita.

“Ni jukumu letu pia kuhakikisha mitaro na maeneo yanayopitisha maji hayajazibwa. Tukisubiri serikali pekee, tunaweza kuchelewa,” amesema.

Mwisho.





Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani.Picha na Samwel Mwanga


Post a Comment

0 Comments