Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano akifungua kongamano la vijana katika wilaya hiyo.Picha na Samwel Mwanga
Samwel Mwanga, Maswa.
VIJANA katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wameshauriwa kuacha tabia ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii na mifumo ya kidijitali, badala yake waitumie kama nyenzo ya kutafuta fursa za mafunzo, ajira na biashara zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza Julai 24,2026 Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano, wakati akifungua Kongamano la Vijana Wilaya ya Maswa lililofanyika wilayani humo, lenye kaulimbiu isemayo "Vijana Tuyajenge, Tanzania Ni Yetu Sote"amesema kuwa ni vizuri mitandao ya kijamii itumike kuwainua kiuchumi.
Amesema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kubadili maisha ya vijana wengi ikiwa wataamua kuitumia kujifunza ujuzi, kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kuanzisha biashara kupitia majukwaa ya kidijitali.
"Mitandao ya kijamii isiwe sehemu ya kupoteza muda au kusambaza taarifa zisizo na manufaa. Itumieni kujifunza, kutafuta masoko ya bidhaa zenu na kuanzisha biashara zitakazowaongezea kipato," amesema.
Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuwataka kutumia fursa zinazotolewa ili kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme, alisema kongamano hilo linalenga kuwaunganisha vijana ili kujadili masuala muhimu yanayogusa maisha yao na maendeleo ya taifa.
Afisa Maendeleo ya jamii wilaya ya Maswa,Hollo Ngeme akizungumza katika kongamano la vijana wilayani humo.Picha na Samwel MwangaAlitaja baadhi ya mada zilizojadiliwa kuwa ni utawala bora, elimu ya uraia, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, fursa za kiuchumi, mapambano dhidi ya rushwa, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, alisema kongamano hilo limewakutanisha vijana zaidi ya 300 kutoka kata zote 36 za wilaya hiyo.
Mtipa amesema lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika maamuzi ya maendeleo, kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao pamoja na kuwahamasisha kutumia maarifa wanayopata kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla.
Mshiriki wa kongamano hilo, Neema Joseph kutoka Kata ya Nyalikungu, amesema mafunzo aliyoyapata yamempa mtazamo mpya kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii.
"Nimegundua kuwa simu niliyokuwa nikiitumia kwa burudani pekee inaweza kuwa chanzo cha kipato. Nitaanza kuitumia kutafuta mafunzo na kutangaza biashara ndogo ninayofanya."amesema.
Naye Juma Jongela kutoka Kata ya Sola amesema kongamano hilo limewapa vijana hamasa ya kujitegemea badala ya kusubiri ajira.
"Tumeelezwa namna ya kutumia teknolojia kupata wateja na kuanzisha biashara. Haya ni maarifa muhimu ambayo yatatusaidia kupunguza ukosefu wa ajira."amesema.
Kwa upande wake, Asha Mohamed kutoka Kata ya Senani amesema elimu kuhusu rushwa, dawa za kulevya na ukatili wa kijinsia imewafungua macho vijana wengi.
"Sisi vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa. Tukitumia mitandao vizuri na kuzingatia maadili, tunaweza kujenga uchumi wetu na kuchangia maendeleo ya Wilaya ya Maswa na Tanzania kwa ujumla."amesema.
Mwisho.







0 Comments