Sehemu ya jengo la kituo cha Afya Sangamwalugesha wilaya ya Maswa kilichofunguliwa na Mwenge wa Uhuru. Picha na Samwel Mwanga.Na Samwel Mwanga, Maswa
ZAIDI ya wananchi 10,000 wa Kata ya Sangamwalugesha wilayani Maswa, mkoani Simiyu, wanatarajiwa kunufaika na huduma za upasuaji na huduma nyingine muhimu za afya baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Sangamwalugesha kilichogharimu Sh 250 milioni.
Akizungumza julai 27, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano, amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya juhudi za serikali za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kupunguza umbali waliokuwa wakisafiri kufuata matibabu.
Amesema kabla ya ujenzi wa kituo hicho, wananchi walikuwa wakilazimika kusafiri kilomita 14 kwenda Kituo cha Afya Lalago kwa ajili ya kupata huduma za upasuaji na huduma nyingine za kibingwa.
"Serikali ilitoa Shiligi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki. Ujenzi ulianza Novemba 28, 2025 na kukamilika Julai 15, 2026. Kukamilika kwake kutawanufaisha zaidi ya wananchi 10,000 wa Sangamwalugesha na maeneo jirani," amesema.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang'onda, ameweka jiwe la msingi la kituo hicho na kuiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kuhakikisha ndani ya siku 14 kituo hicho kinaanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa,Wazo Mwang'onda (aliyetangulia)akikagua sehemu ya jengo la lituo cha Afya Sangamwalugesha wilaya ya Maswa. Picha na Samwel MwangaMwang'onda amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika kuboresha sekta ya afya, hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanaanza kupata huduma bila kuchelewa.
Aidha, amewataka wananchi kushiriki kulinda na kutunza miundombinu ya kituo hicho ili idumu na kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
"Halmashauri ihakikishe ndani ya siku 14 wananchi wanaanza kupata huduma. Wakati huo huo, wananchi walinde miundombinu hii kwa sababu imejengwa kwa fedha za umma kwa ajili ya kuwahudumia wao," amesema.
Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutapunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu, hususan kwa wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Naano(mwenye kipaza sauti)akieleza juu ya ujenzi wa kituo cha Afya Sangamwalugesha. Picha na Samwel MwangaMkazi wa Sangamwalugesha, Neema Magesa, amesema wanawake wajawazito walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa kufuata huduma za afya kutokana na umbali.
"Tulikuwa tunasafiri umbali mrefu kwenda Lalago. Wakati mwingine mama mjamzito alikuwa anaanza uchungu usiku na usafiri unakuwa tatizo. Sasa tunaamini maisha ya wengi yataokolewa kwa kuwa huduma zipo karibu," amesema.
Naye Mariam Manyanda amesema ujio wa kituo hicho utapunguza gharama ambazo familia zilikuwa zinatumia kufuata matibabu.
"Tulikuwa tunatumia fedha nyingi kwa usafiri na muda mwingi njiani. Sasa tutapata huduma kwa haraka na fedha hizo tutazielekeza kwenye maendeleo ya familia," amesema.
Kwa upande wake, John Shija amesema wananchi wana wajibu wa kutunza kituo hicho ili kiweze kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
"Tunamshukuru Rais na Serikali kwa kutuletea huduma hizi. Sasa tunachohitaji ni watumishi wa kutosha, dawa na vifaa tiba ili kituo hiki kifanye kazi kwa ufanisi na kutimiza matarajio ya wananchi," amesema.
Kukamilika kwa Kituo cha Afya cha Sangamwalugesha kunatajwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha huduma za afya katika Wilaya ya Maswa, huku kikitarajiwa kupunguza rufaa zisizo za lazima na kusogeza huduma za upasuaji na matibabu mengine muhimu karibu na wananchi.
Mwisho.
0 Comments