RC SIMIYU AONYA WATAKAOVURUGA AMANI.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

Na Mwandishi wetu.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amewahakikishia Wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa huo uko salama na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama  vimejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi na mali zao vinalindwa wakati wote.

Akizungumza leo, tarehe 6 Julai 2026, katika Baraza Maalum la Madiwani lililokutana kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kujaribu kuvuruga amani ya mkoa huo.

Amewataka Madiwani pamoja na viongozi wa ngazi zote  kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinaendelea kudumishwa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya mkoa.

Aidha, amewahimiza wananchi kuunga mkono dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha amani na usalama Nchini.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapobaini viashiria vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani, akieleza kuwa ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kulinda usalama wa jamii.

Mwisho.



Post a Comment

0 Comments