NIRC YATANGAZA MKAKATI MPYA KUSAMBAZA MITAMBO YA VISIMA VIREFU NCHINI.


Na Mwandishi wetu.

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, ametangaza mkakati wa kusafirisha mitambo mikubwa ya kuchimba visima virefu kwenda mikoa yenye changamoto ya upatikanaji wa maji chini ya ardhi mara baada ya kukamilisha kazi katika shamba la BBT Chinangali mkoani Dodoma.

Mndolwa ameiagiza Idara ya Mitambo ya NIRC kufanya tathmini ya namna salama ya kusafirisha mitambo hiyo bila kuharibu miundombinu ya barabara, ikiwemo uwezekano wa kuifungua katika sehemu mbalimbali ili kupunguza uzito wakati wa usafirishaji.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) Chinangali, alisema hatua hiyo itaiwezesha NIRC kupeleka huduma za uchimbaji wa visima kwa ufanisi zaidi katika maeneo yanayokabiliwa na ukame na uhaba wa maji.

Katika ziara hiyo, Mndolwa alikagua ujenzi wa barabara za ndani, mabwawa, uchimbaji wa visima na uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji. Pia alitembelea mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kuchimba visima hadi mita 1,800 chini ya ardhi, ambao kwa sasa unachimba visima viwili vya mwisho kati ya visima 40 vinavyojengwa katika shamba hilo.

Ziara hiyo ilihudhuriwa na wataalamu mbalimbali wa NIRC, akiwemo Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu, Mhandisi Leopard Runji, Mhandisi wa Mkoa wa Dodoma, Oswald Urassa, pamoja na Muendesha Mitambo ya Visima Virefu, Mosses Mkude.

Mwisho.










Post a Comment

0 Comments