MASWA YAJIPANGA KUKABILI MABADILIKO YA TABIANCHI KUPITIA MRADI WA SCALE.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akizungumza katika kikao cha kuwajengea uwezo madiwani juu ya mradi wa mabadilko ya tabianchi. Picha na Samwel Mwanga

Na Samwel Mwanga, Maswa

HALMASHAURI ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeanza utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Programu ya SCALE, inayolenga kuongeza ustahimilivu wa jamii na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Akizungumza leo Julai 2, 2026, katika kikao cha kuwajengea uwezo madiwani kuhusu utekelezaji wa programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia, ikiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Programu ya SCALE inatekelezwa katika halmashauri 54 nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, ambapo kata 12 zitafaidika. Kata hizo ni Lalago, Sukuma, Isanga, Masela, Dakama, Mbaragane, Seng'wa, Buchambi, Binza, Kadoto, Badi na nyingine iliyopangwa ndani ya utekelezaji wa programu.

Mtipa amesema programu hiyo ya miaka mitano inatumia mfumo wa "malipo kwa matokeo" (Results-Based Financing), ambapo kiwango cha fedha kitakachotolewa kitategemea namna halmashauri itakavyotekeleza shughuli zake kwa kuzingatia masharti na kufikia matokeo yaliyokusudiwa.

Sehemu ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao cha kujengewa uwezo wa mradi wa mabadiliko ya tabianchi. Picha na Samwel Mwanga.

"Kadiri tutakavyotekeleza vizuri programu kwa kufuata masharti na kufikia malengo yaliyowekwa, ndivyo tutakavyopata fedha zaidi za kuendeleza utekelezaji wake. Hadi sasa Halmashauri ya Maswa imepokea Sh72.9 milioni kwa ajili ya kuanza shughuli za awali za programu," amesema Mtipa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya SCALE wilayani humo, Julius John, amesema mafanikio ya utekelezaji wake yatategemea ushiriki wa wananchi, hususan katika kuibua na kushughulikia malalamiko yanayohusu athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema upembuzi yakinifu uliofanyika umebaini kuwa jamii ina uhitaji mkubwa wa miradi ya maji, uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nishati safi na hatua za kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Mratibu wa program ya Scale halmashauri ya wilaya ya Maswa,Julius John akizungumza katika kikao cha kuwajengea madiwani wa halmashauti hiyo juu ya program hiyo. Picha na Samwel Mwanga

Kwa mujibu wake, miradi iliyopewa kipaumbele ni pamoja na uchimbaji na ufufuaji wa visima, ujenzi wa mabwawa madogo (dams), ukarabati wa malambo, ujenzi wa mabirika ya maji kwa ajili ya mifugo, upandaji wa mbegu za malisho, matumizi ya nishati mbadala, upandaji miti pamoja na matumizi ya mbegu na pembejeo zinazostahimili ukame.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji, kuboresha sekta za kilimo na mifugo, kulinda mazingira na kuchochea maendeleo endelevu katika halmashauri hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Miza Jishuli, ameishukuru Serikali kwa kuiletea halmashauri hiyo programu ya SCALE, akisema utekelezaji wake unapaswa kuzingatia vipaumbele vilivyoainishwa na wananchi ili uwe na manufaa yaliyokusudiwa.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Miza Jishuli akizungumza wakati wa kikao cha mradi wa mabadiliko ya tabianchi. Picha na Samwel Mwanga

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Zanzui, Witness Philipo, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa programu hiyo ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha yao.

Mwisho.

Sehemu ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao cha kujengewa uwezo wa mradi wa mabadiliko ya tabianchi. Picha na Samwel Mwanga


Post a Comment

0 Comments