DK. LUGOMELA AFANYA ZIARA NG'WIGWA NA SUKUMA, WANANCHI WAPONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO.

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Mashariki, Dkt. George V. Lugomela, akizungumza kwenye Mkutano wa Hadhara.

Na Mwandishi wetu, Maswa.

MBUNGE wa Jimbo la Maswa Mashariki, Dkt. George V. Lugomela, ameendelea na ziara yake ya Kata kwa Kata yenye lengo la kuwashukuru wananchi wa Kata za Ng’wigwa na Sukuma, kutokana na imani waliyoionyesha kwa kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye kama Mbunge, pamoja na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi.

Akiwa katika Kata ya Ng’wigwa, Dkt Lugomela pamoja na wananchi, wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo unaoendelea katika eneo lao ili kuwaletea Maendeleo.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika Shule ya Msingi Suligi wenye thamani ya shilingi Mil. 135, ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi Ng’wigwa wenye thamani ya shilingi Mil 330, ujenzi wa darasa moja katika Shule ya Msingi Mwasita wenye thamani ya shilingi Mil. 10.76 pamoja na kutiwa saini kwa mradi wa maji wa Mwasita na Mwabayanda wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bil. 2.1.

Kwa upande wa Kata ya Sukuma, wananchi wameipongeza Serikali kwa kukamilisha miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Sekondari mpya ya Isageng'he, Tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni mbili, pamoja na awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa yenye thamani ya shilingi Mil. 70.

Wakizungumza katika mikutano hiyo, Madiwani wa kata hizo, Steven Dwese (Ng’wigwa) pamoja na Mary Misangu (Sukuma), wamepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo. 

Aidha, Madiwani hao wamemshukuru Dkt. Lugomela, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushirikiano unaoendelea kuharakisha maendeleo katika Jimbo la Maswa Mashariki.

Kwa upande wake, Dkt. George V. Lugomela amewashukuru wananchi wa Maswa Mashariki kwa kuendelea kudumisha amani, mshikamano na utulivu, akisisitiza kuwa ushirikiano wao ni nguzo muhimu katika kuendeleza maendeleo ya jimbo hilo.

Mwisho.




Post a Comment

0 Comments