Na Mwandishi wetu.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Bariadi chini ya Mkurugenzi wake, Iddi Ndabhona, pamoja na Menejimenti ya Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ulioiwezesha Halmashauri kukusanya asilimia 100.15 ya lengo la mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Macha ametoa pongezi hizo leo Julai 6, 2026, wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa kupokea na kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na kwa wakati ili kupunguza hoja zinazotokana na uzembe na kuhakikisha Halmashauri inafikia lengo la kufunga hoja zote za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Iddi Ndabhona, kwa uongozi madhubuti ulioongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka asilimia 87 katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi kufikia asilimia 100.15 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Iddi Ndabhona, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutambua juhudi za Halmashauri na kuahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa umakini ili kuhakikisha hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinafungwa na kuimarisha zaidi uwajibikaji pamoja na maendeleo ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Mwisho.










0 Comments