VIKUNDI SITA VYANUFAIKA NA MKOPO WA SHILINGI MIL. 89 MASWA.


Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk. Vicent Naano (wa pili kulia) akikabidhi mfano wa hundi kwa kiongozi wa kikundi cha walemavu, Grace Geoge (wa kwanza kushoto aliye mbele) katika hafla ya kukabidhi mikopo kwa makundi maalum wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga

Na Samwel Mwanga, Maswa.

VIKUNDI  sita vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, vimenufaika na mkopo wa jumla ya Sh 89 milioni unaotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya kuyawezesha makundi maalumu kiuchumi.

Vikundi hivyo vinajumuisha kikundi kimoja cha wanawake kilichopata mkopo wa Sh 10 milioni, vikundi vinne vya vijana vilivyopata jumla ya Sh 76 milioni na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu kilichopata Sh 3 milioni.

Akizungumza juni 24,2026 wakati wa hafla ya kukabidhi hundi za mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme, amesema fedha hizo zimetolewa katika robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema kati ya fedha hizo, sehemu imetokana na mapato ya ndani ya halmashauri, huku Sh 43 milioni zikitokana na marejesho ya mikopo iliyotolewa awali kwa vikundi mbalimbali.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo kupitia makundi maalum katika halmashauri ya wilaya ya Maswa walioshiriki hafla ya utoaji mikopo.Picha na Samwel Mwanga

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa uadilifu kwa kuendeleza shughuli walizoziombea mikopo na kuhakikisha wanarejesha kwa wakati kwa mujibu wa mikataba yao.

Amesema vikundi vinavyojihusisha na shughuli za uzalishaji mali kama ufyatuaji wa matofali, uchomeleaji vyuma na utengenezaji wa madirisha ya vioo vinapaswa kujisajili ili viweze kupewa kipaumbele cha zabuni na kazi mbalimbali zitakazotolewa na halmashauri.

"Tunataka vikundi hivi vikue kiuchumi na viwe sehemu ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika halmashauri yetu. Kujisajili kutawapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika kazi mbalimbali zinazojitokeza," amesema.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga

Akikabidhi hundi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Vicent Naano, alivitaka vikundi vilivyonufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili fedha hizo ziweze kuwafikia wananchi wengine wenye uhitaji.

Aidha, aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia vikundi vyote ambavyo vimeshindwa kurejesha mikopo kwa wakati ili hatua stahiki zichukuliwe na fedha za umma zilindwe.

"Fedha hizi si sadaka bali ni mikopo ya serikali inayolenga kuyawezesha makundi maalumu. Lazima irejeshwe kwa wakati ili wananchi wengine pia wapate fursa ya kunufaika," amesema.

Amesema zaidi ya Sh 700 milioni zilizowahi kutolewa kama mikopo na halmashauri hiyo bado hazijarejeshwa, hali inayokwamisha juhudi za kuwafikia wanufaika wengine.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga.

Dk Naano alibainisha kuwa baadhi ya vikundi vya vijana vimekuwa vinara wa kuchelewesha marejesho ya mikopo na kuvitaka kubadilika ili programu hiyo iendelee kuwa na manufaa kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Jumilage Maiko kutoka Kikundi cha Vijana cha Mshikamano kilichopo Kijiji cha Mwanghonoli, alisema mkopo walioupata utawawezesha kuongeza vifaa vya uchomeleaji na kupanua huduma zao.

"Tunamshukuru Rais na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa kutupatia mtaji huu. Tutautumia kuongeza uzalishaji na kuajiri vijana wengine. Tunaahidi kurejesha mkopo kwa wakati ili vikundi vingine navyo vipate nafasi ya kunufaika," amesema.

Naye Emaculata Joseph kutoka Kikundi cha Amani katika Kijiji cha Mwabagalu alisema mkopo huo utasaidia kukuza biashara zao na kuongeza kipato cha familia zao.

"Fedha hizi zimekuja wakati muafaka. Tutaziwekeza katika shughuli tulizoziwasilisha kwenye maombi yetu na kuhakikisha tunafanya marejesho kwa wakati. Tunaamini zitatusaidia kujikwamua kiuchumi," amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Watu Wenye Ulemavu cha Amani katika Kijiji cha Isanga, Grace George, alisema mkopo huo ni fursa muhimu kwa watu wenye ulemavu kujiongezea kipato na kujitegemea.

"Kwa muda mrefu tumekuwa tukihitaji mtaji wa kuendesha shughuli zetu. Mkopo huu utatusaidia kupanua miradi yetu na kuboresha maisha ya wanachama wetu. Tunaahidi kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuurejesha kwa wakati," amesema.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments