TINA CHENGE ACHANGIA BAJETI KUU YA SERIKALI, AZUNGUMZIA PAMBA, BARABARA, UTALII NA UMEME.

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, Tina Chenge, akichangia mjadala wa Bajeti Bungeni jijini Dodoma leo Juni 21, 2026.


Na COSTANTINE MATHIAS, Dodoma.

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, Tina Chenge, ameitaka Serikali kuondokana na mfumo wa kusafirisha malighafi kwenda nje bila kuongezwa thamani na badala yake kuelekeza nguvu katika uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yamebainishwa leo na Mbunge huyo wakati akichangia Bajeti Kuu ya serikali Bungeni jijini Dodoma, ambapo amesema Mkoa wa Simiyu unazalisha zaidi ya asilimia 55 ya pamba yote nchini, lakini hadi sasa hakuna kiwanda cha kuchakata pamba ndani ya mkoa huo. Amesema hali hiyo husababisha pamba kusafirishwa kama malighafi kwenda maeneo mengine huku wananchi wa Simiyu wakikosa fursa za kunufaika zaidi na rasilimali hiyo.

Amesema katika kila msimu wa mavuno, malori mengi huonekana yakisafirisha pamba kuelekea Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya masoko na uchakataji katika maeneo mengine, jambo linalowaacha wananchi wa Simiyu kama watazamaji huku bei ya pamba ikiendelea kuamuliwa na soko la dunia bila wao kuwa na ushawishi mkubwa.

Chenge amesema uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata pamba ndani ya Simiyu utasaidia kuongeza thamani ya zao hilo, kuzalisha ajira kwa vijana na wanawake, kuimarisha mapato ya mkoa pamoja na kuboresha bei na kipato cha wakulima wa pamba. Aidha, ameitaka Serikali na sekta binafsi kushirikiana kuwekeza katika uchakataji wa mazao ili kuchochea maendeleo ya viwanda na uchumi wa wananchi.

Katika hatua nyingine, Tina Chenge amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi ya Kimkakati ikiwemo Mradi wa kufua Umeme, Daraja la Kigongo Busisi, Mradi wa Reli ya Kisasa ambao unaendelea kujengwa katika maeneo yaliyobakia na endapo ukikamilika utakuza uchum, kukuza ajira kwa sekta rasmi na isiyo rasmi Kwa Wanawake na vijana. 

‎Amesema kuwa kuna vivutio ambayo havijatangazwa ikiwemo maporomoko ya Kalambo, Kisasa, Ngorongoro huku akiisisitisa serikali kutangaza vivutio hivyo ili kuongeza pato la serikali kupitia sekta ya Utalii, huku akiwapongeza Mawaziri, Manaibu Mawaziri pamoja na watendaji wao kwa kuja na Bajeti jumuishi na ya kizalendo ambayo Utekelezaji wake kwa asilimia 74 utagharamiwa na pato la ndani.

Sikiliza hapa chini...




Post a Comment

0 Comments