Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu kimeitaka serikali kuondoa vikwazo na kuanza mara moja ununuzi wa zao la Pamba ili wananchi waweze kunufaika na jasho lao.
Imeelezwa kuwa licha ya serikali kufanya Uzinduzi Mei 10, 2026 pamoja na kutangaza bei elekezi ya shilingi 1,240/= kwa kilo moja katika Kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga Mkoani Tabora, Wanunuzi wa Pamba bado hawajaanza kununua zao hilo kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo vibali na mizani.
Akizungumza leo Juni 4, 2026 na Waandishi wa Habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Simiyu, Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Lumen Mathias alisema CCM Mkoa wa Simiyu imeadhimia kuwa ifikapo Juni 6, 2026 zao la Pamba lianze kununuliwa katika Mkoani huo.
"Kuna changamoto ya ununuzi wa zao la pamba, bado kuna changamoto ya Ununuzi wa Pamba, Kamati ya siasa ya Mkoa wa Simiyu inaielekeza serikali ifikapo tarehe 6/6/2026, zao la pamba liwe limeanza kununuliwa kwa wakulima wetu wa mkoa wa Simiyu" amesema Mwenezi na kuongeza.
"Kuna changamoto katika uzalishaji na wakulima wanawekeza fedha nyingi katika Kilimo cha pamba, tunahitaji zao hilo lianze kununuliwa...Kamati ya siasa inaielekeza serikali kuruhusu ununuzi wa zao hili, Chama tumefuatilia mizani ambayo mwaka huu itatumika ilikuwa inampunja kilo 20 na serikali ilifanya jitihada za kurudisha mizani hiyo ili isimpunje mkulima".
Alisema kutoanza kununua Pamba ni kuigombanisha serikali na Wananchi ambao wameipa CCM madaraka na kwamba baadhi ya Wanunuzi walikuwa na mikataba mya kuhudumia kata si rafiki na wakati ujao ushindani utazingatiwa katika Mkoa wa Simiyu.
Kuhusu Ucheleweshaji wa Malipo ya Wakulima, Mwenezi huyo amewaomba Wanunuzi wa Pamba kuwatendea haki wakulima ili wapate haki yao kwa wakati huku akiwasisitiza Makampuni ya Pamba kulipa ushuru na tozo za serikali ili kuharakisha Maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa jumla.
Mwisho.





0 Comments