Moja ya shamba la Pamba ambalo limepasuka tayari kwa uvunaji katika mtaa wa Diana, kata ya Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
KUTOKANA na Pamba ya Tanzania kuonyesha kiwango kidogo cha Ubora katika Soko la dunia, Wakulima wa Pamba wilayani Bariadi Mkoani Simiyu, wamesisitizwa kuvuna mapema na kuhifadhi pamba mahali salama ili kulinda ubora na Usafi wa Pamba hali itakayochangia kuimarisha soko la zao hilo muhimu wa kiuchumi nchini.
Imeelezwa kuwa katika msimu miwili ya 2024/2025, viwango vya ubora wa Pamba ya Tanzania vilishuka na kufikia asilimia 7 lakini msimu wa 2025/2026 viwango vya Ubora vilipanda na kufikia asilimia 21 huku lengo la serikali ni kufikia asimilia 50 ya ubora msimu 2026/2027.
Hayo yamebainishwa jana na Afisa Kilimo kutoka Bodi Pamba ambaye ni Mtaalamu wa Maabara, Usafi na Ubora wa Pamba Kanda ya Shinyanga, Penina Range, wakati akitoa elimu ya Usafi na Ubora wa Pamba kwenye Mkutano uliokutanisha BBT, viongozi wa Amcos na wataalamu kutoka Bodi ya Pamba.
Aidha, Viongozi wa vyama vya Ushirika (Amcos) pamoja na Maafisa Kilimo kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT) wamesisitizwa kusimamia na kukagua ubora wa Pamba kabla haijauzwa sokoni.
Mtaalamu huyo aliwataka BBT na Viongozi wa Amcos kuumarisha Usimamizi katika Usafi na Ubora wa Pamba ili kupata Pamba ubora itakayoshindanishwa kwenye soko la dunia.
"Sote tuungane kukagua ubora wa Pamba, tunahitaji kununua Pamba safi na kusimamia ubora, viwango vya ubora vinaongezeka lakini pia tusimamia wakulima wapewe bei iliyoko sokoni na mabango ya bei yabandikwe kwa wakati" amesema.
Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Bariadi, Anthony Ndinda aliwataka BBT na Viongozi wa Amcos kusimamia ubora wa pamba pamoja na maslahi ya wakulima huku akisisitiza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha wakulima hawaibiwi kwa namna yoyote.
"Tumejipanga kuhakikisha wakulima hawaibiwi, yoyote akitaka kuchezea mzani utazima hapohapo, lakini pia tunaendelea kuwapatia wakulima Elimu ya ugani na tunatarajia kila mdau akatimize Wajibu wake katika kulinda ubora wa pamba" amesisitiza.
Aliwataka viongozi wa Amcos na BBT kutotengeneza matabaka pamoja na kubaguana huku akiwasisitiza kufanya kazi kama timu moja ili kuhakikisha mkulima anapata alichostahili kutokana ana jasho lake.
Afisa Ugani kupitia Mpango wa Jenga Kesho (BBT) kutoka kata ya Ikungulyabashashi, Mariam Ismail alisema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa kusimamia ubora wa Pamba wakishirikiana na viongozi wa Amcos.
Alisema kutokana Elimu waliyopata, watahakikisha katika msimu huu pamba itakuwa safi kuliko misimu iliyopita huku akisisitiza kuwa awataendelea kuelimisha wakulima wa pamba juu ya faida na hasara za kuchafua pamba.
Naye, Naivester Anosisye, BBT kutoka kata ya Dutwa alisema wanashirikiana na wakulima kutoa elimu tangu kuandaa shamba, upandaji, unyunyiziaji, uvunaji hivyo anaamini wataendelea kuelimisha wakulima hao kuhusu Usafi na Ubora wa Pamba ili kukidhi soko la kimataifa.










0 Comments