TAHARUKI SIMIYU; POLISI WAMNUSURU MWANAMKE KWA TUHUMA ZA UCHAWI.

Na Mwandishi wetu.

JESHI la Polisi Mkoa wa Simiyu leo Mei 14, 2026 majira ya mchana, limefanikiwa kumuokoa mwanamke mmoja katika eneo la Mtaa wa Kidinda baada ya kuzungukwa na kundi la wananchi waliokuwa wakimtuhumu kuwa ni mchawi kwa lengo la kumshambulia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa eneo la tukio, mwanamke huyo alikuwa akipita njiani ambapo alikutana na binti mmoja na kuanza kumzunguka. Baada ya muda mfupi, binti huyo alidaiwa kuishiwa nguvu hali iliyosababisha wananchi waliokuwepo eneo hilo kuanza kumtuhumu mwanamke huyo kuhusika na vitendo vya kishirikina.

Binti huyo alikimbizwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu, ambapo madaktari walibaini kuwa alikuwa yupo salama.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limetoa wito kwa wananchi kuacha kuamini na kuendeleza imani za kishirikina ambazo hazina ukweli wala uthibitisho wa kisayansi. Polisi wameeleza kuwa imani hizo zimekuwa chanzo cha matukio mbalimbali ya mauaji, majeruhi, migogoro na kusambaratika kwa familia katika jamii.

Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, likisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria. Polisi wameonya kuwa hawatasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu au kundi lolote litakalokiuka sheria na taratibu za nchi.


Mwisho.







Post a Comment

0 Comments