Wanawake wakiwa kwenye shughuli za biashara.

Biashara ndogo zisizo rasmi zinavyookoa familia huku mchango wao ukibaki kivulini.

Na Samwel Mwanga, Simiyu.

ASUBUHI inapochomoza katika masoko, minadani na pembezoni mwa barabara za mkoa wa Simiyu, wanawake wengi huanza siku zao mapema wakipanga nyanya, vitunguu, dagaa, maandazi, mboga, nafaka na bidhaa nyingine ndogo ndogo.

Kwa wengi, hizi si biashara za pembeni, Ndizo nguzo za uchumi wa familia.

Katika mkoa ambao wananchi wengi hutegemea kilimo na mifugo, wanawake kupitia biashara ndogo zisizo rasmi wameendelea kubeba sehemu kubwa ya uchumi wa kaya mara nyingi bila kutambuliwa ipasavyo katika mijadala ya uchumi.

Hali hali inaonyesha katika wilaya za Maswa, Bariadi, Meatu, Busega na Itilima, mamia ya wanawake huendesha biashara ndogo zinazosaidia kulipia chakula, ada za watoto, matibabu na mahitaji ya kila siku.

Uchumi unaobebwa kwa mikono katika masoko ya vijijini na mijini midogo, wanawake huuza kila kitu kuanzia mbogamboga, samaki wa kukaanga, vitafunwa, maziwa, nafaka hadi bidhaa za rejareja.

Wengine huzunguka mitaani kuuza bidhaa kichwani,wengine huendesha vibanda vidogo na wengine hujiongezea kipato kwa kusindika mazao kama unga, karanga au mafuta ya alizeti.

Lakini pamoja na udogo wa biashara hizo, mchango wake kwenye maisha ya familia ni mkubwa.

“Mama wengi ndiyo wanashikilia matumizi ya kila siku ya nyumbani,” anasema John Hangwa ambaye ni mchambuzi mmoja wa maendeleo ya jamii Simiyu.


Biashara ndogo, mchango mkubwa.

Katika kaya nyingi, mapato ya biashara hizi ndogo ndiyo yanaziba pengo pale kilimo kinapodorora, mavuno yanapokuwa duni au bei za mazao kushuka.

Kwa baadhi ya familia, kipato cha mama kutokana na biashara ndogo ndicho kimewezesha watoto kusoma, familia kupata chakula na hata kujenga nyumba.

Lakini kwa kuwa biashara hizi ziko kwenye sekta isiyo rasmi, mchango wake mara nyingi hauonekani wazi katika takwimu za uchumi.


Changamoto zisizoonekana.

Pamoja na umuhimu wao, wanawake hawa hukabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na mitaji midogo na faida ndogo.

Wapo wanaouza bila vibali rasmi, wengine wakikabiliwa na tozo ndogo ndogo,ushindani mkubwa na ukosefu wa maeneo salama ya biashara.

Wengine huendesha biashara huku wakibeba majukumu mengine ya kulea familia.

“Anatakiwa kuuza, apike, alee watoto, asimamie nyumba. Mzigo ni mkubwa,” anasema Slivester Lugembe mkazi wa mjini Maswa.

Mikopo bado ni kikwazo.

Wengi wa wanawake hawa hawana dhamana za kupata mikopo mikubwa benki, na hata pale fursa zinapokuwepo, taarifa au masharti huwafanya wengi kubaki nje ya mfumo.

Wadau wa uchumi jumuishi wanasema wanawake wa biashara ndogo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa chini, lakini bado hawajapatiwa mazingira rafiki ya kukua.


Sekta isiyo rasmi inayobeba Simiyu.

Katika mkoa wa Simiyu, ambako sehemu kubwa ya shughuli za uchumi ziko kwenye sekta isiyo rasmi, mchango wa wanawake hawa ni mkubwa kuliko unavyoonekana.

Ni wao wanaosukuma biashara za sokoni.

Ni wao wanaounganisha uzalishaji wa mashambani na matumizi ya majumbani.

Ni wao wanaofanya uchumi wa kaya usianguke.Lakini mara nyingi kazi hiyo hufanyika kimya kimya bila kutambuliwa na bila kulindwa vya kutosha.


Wito wa kuwawezesha.

Wachambuzi wa maendeleo wanasisitiza kuwa kuwawezesha wanawake hawa si suala la ustawi wa familia pekee, bali ni mkakati wa kukuza uchumi wa mkoa.

Wanashauri kuongeza upatikanaji wa mitaji, maeneo bora ya biashara, mafunzo ya ujasiriamali na kupunguza vikwazo vinavyowakwamisha.

Kwa sababu nyuma ya vibanda vidogo, vikapu vya sokoni na biashara za mitaani, kuna uchumi mkubwa unaobebwa na wanawake.

Na katika Simiyu, wanawake wengi si washiriki wa pembeni wa uchumi ni waubebaji wake wakuu.

MWISHO.