Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Renatus Luneja akizungumza kwenye Uzinduzi wa Msimu wa ununuzi wa Pamba 2026/2027.
Na COSTANTINE MATHIAS, Igunga.
Akizungumza jana kwenye Uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba, uliofanyika kijiji cha Mwamashimba wilayani humo, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Renatus Luneja amesema kuwa Serikali imeshatoa fedha Kwa ajili ya ujenzi wa Mradi huu, wakati huo wilaya ya Igunga imetoa eneo katika Kijiji cha Mbutu kwa ajili ya kuanza ujenzi.
"Kabla ya mwaka huu haujaisha kutajengwa kiwanda cha kuchakata mbegu za pamba, tumeshapata eneo pale Mbutu, Serikali imetoa fedha na mchakato unaendelea na kiwanda kitasimikwa hapo...Wakulima wa Igunga watakuwa na uwezo wa kutekeleza hitaji la kupewa Bei ya ziada sababu wanazalisha mbegu kwa mfumo rasmi." Amesema Luneja.
Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Tabora, Mrisho Mandali amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya kaguzi za kushitukiza ili kubaini wanaochezea mizani kwa ajili ya kuwapunja wakulima wa Pamba.
Amesema kuwa mizani iliyotumika mwaka jana imeboreshwa ili kuongeza ulinzi katika mizani hiyo ikiwemo swichi inayozima wakati ikibainika kuchezewa kwa lengo la kulinda mkulima na mnunuzi.
"Tukikutana na changamoto ya uchakachuaji wa mizani, hiyo ni jinai, mhusika akikiri Kuna kiwango cha faini mpaka shilingi Mil. 1, pamoja na kupelekwa mahakamani, lakini mwaka huu tumedhamiria kuwapeleka mahakamani wote watakaobainika kuchezwa mizani" amesema Mrisho
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, AnaMringi Macha aliwataka wakulima wa Pamba kuzingatia Ushauri wa Maafisa Ugani ili waweze kuzalisha kwa tija na kwamba serikali ya Rais Dk. Samia haiwezi kuleta jambo ambalo halina maslahi kwa wakulima na Wananchi wake.
'Mwendo ni hatua, mwaka jana bei ilikuwa 1150 na mwaka huu bei ni 1240, Kuna ongezeko la asilimia 8, ambayo imeonekana Kwa wakati huu...hii Pamba tunayolima asilimia 70 inauzwa nje na asilimia 30 tutatumia ndani, soko la kule ndio tunalitegemea, na sababu ya serikali kuweka Bei elekezi ni kulinda wakulima wasinunuliwe pamba yao kwa Bei ya chini".
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Sauda Mtondoo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga amesema serikali itaendelea kusimamia mfumo wa Malipo ya wakulima na kwamba itazifanyia kazi changamoto ili mkulima aweze kufurahia jasho lake.
"Msimu wa ununuzi wa pamba 2026/2027 umefunguliwa rasmi leo na Bei elekezi ya kununulia Pamba itakuwa shilingi 1,240/= kwa kilo moja ya pamba ya daraja A na shilingi 620 daraja B, naeleekeza taratibu zote zingatiwe...wakulima walipwe kwa wakati na haki itendele kwa kila mdau" amesema.
Kwa upande wao wakulima wameipongeza serikali kuja na mabadiliko ya bei kutoka 1,150/= ambayo ilikuwa bei elekezi ya msimu 2025/2026 na kufikia 1,240/= msimu wa 2026/2027.
Tatu Shija, mkulima wa kijiji cha Mwamashimba
anaishukuru serikali kuongezea bei ya pamba huku akiomba kuwa endapo bei itaongezeka katika soko la Dunia, pia Wanunuzi wawaongezee Bei wakulima wa pamba.
Mwisho.










0 Comments