MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga akizungumza kwenye Mkutano wa Hadhara.

Na Mwandishi wetu.

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Simon Simalenga, ametembelea na kufanya Mikutano ya hadhara katika vijiji cha Salalia Kata ya Matongo pamoja na Chungu kata ya Gibishi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya (Simalenga) amezungumzia kwa kina changamoto na madhara ya ujangili pamoja na uvamizi wa Tembo katika maeneo ya ya Makazi ya wananchi na kueleza kuwa Serikali ya Rais. Dk. Samia inaendelea na ujenzi wa fensi ya umeme ikiwa ni sehemu ya kudhibiti wanyama hao kuingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi.


Aidha, amewasisitiza wananchi kutumia Teknolojia ya kilimo cha pilipili kama njia mojawapo ya kuwafukuza tembo ili wasiharibu mazao yao hususani kipindi hiki cha mavuno huku akibainisha kuwa tembo huogopa harufu kali ya pilipili hivyo mbinu hiyo inaweza kusaidia kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama hao.

Kwa upande wa kilimo, Mkuu huyo wa Wilaya amehimiza wananchi kuendelea na kilimo cha umwagiliaji kwa zaidi ya misimu miwili au mitatu kwa mwaka ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa mazao ili kukabiliana na baa la njaa.

Amesema hatua hiyo itasaidia wananchi kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza kipato cha familia zao, huku akisisitiza pia Kilimo cha mazao ya muda mfupi na yanayaostahimili ukame au mvua kidogo.

Simalenga pia amesema kuwa bwawa la umwagiliaji la Kasoli limefikia asilimia 92 ya utekelezaji, jambo ambalo linatarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika shughuli za kilimo mara litakapokamilika.

Sambamba na hayo, ametoa rai kwa wafugaji kuhakikisha wanaingiza mifugo shambani kwa ajili ya kuongeza rutuba ya ardhi na kuboresha uzalishaji wa mazao, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji kwa maendeleo ya wilaya hiyo.

Wananchi waliohudhuria mikutano hiyo wamepongeza juhudi za Mkuu wa Wilaya kwa kuwafikia moja kwa moja na kusikiliza changamoto zao, huku wakieleza matumaini yao kuwa maagizo na mikakati iliyotolewa itasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu.

Mwisho.