TMDA YATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WAUZAJI NA WAMILIKI MADUKA YA DAWA VIJIJINI.

Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki,Venance Burushi akizungumza wakati wa kikao kazi kati ya TMDA,wamiliki wa Famasi na maduka ya dawa muhimu wilayani Maswa.Picha na Samwel Mwanga.

Na Samwel Mwanga,Maswa.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetakiwa kufika katika maeneo ya vijijini ili kutoa elimu kwa wauzaji na wamiliki wa maduka ya dawa muhimu kuhusu  sheria,taratibu na vigezo  vinavyopaswa kuzingatiwa katika uendeshaji wa maduka hayo ili kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya dawa na kulinda afya za wananchi.

Hayo yameelezwa leo Machi 31,2026 katika kikao kazi kilichowakutanisha TMDA, wamiliki wa famasi na  wamiliki wa maduka ya dawa muhimu katika halmashauri ya wilaya ya Maswa.

James John ni mmiliki wa duka la dawa muhimu mjini Maswa amesema kuwa wamiliki wengi wa maduka katika maeneo ya vijijini hawajui matakwa ya kisheria,jambo linalohatarisha afya za wananchi.

"Licha ya TMDA kufanya kazi kubwa ya kusimamia ubora wa dawa nchini, bado maeneo mengi ya vijijini yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa maduka ya dawa,"amesema.

Baadhi ya wamilili wa famasi na maduka ya dawa muhimu katika wilaya ya Maswa waliohudhuria kikao kazi kati yao na TMDA.Picha na Samwel Mwanga.

Naye James Paschal mmiliki wa duka la dawa muhimu katika kijiji cha Jija wilayani humo amesema kuwa kufika kwa mara kwa mara kwa wataalamu wa TMDA katika vijiji kutasaidia kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa.

Amesema baadhi ya wananchi vijijini bado hununua na kutumia dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya jambo linaloweza kusababisha madhara kiafya.

“Ni muhimu TMDA wakaongeza juhudi za kufika vijijini kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara wa dawa ili kila mtu aelewe matumizi sahihi ya dawa na madhara ya kutumia dawa bila kufuata maelekezo ya wataalamu,” amesema.

Kwa upande wake,Bertha Charles mmiliki wa famasi mjini Maswa amesema kuwa kuna umuhimu wa mamlaka hiyo kufika maeneo ya vijijini mara kwa mara kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa.

"Tunaiomba TMDA ifike huko maeneo ya vijijini kutoa elimu,ukaguzi na kuhakikisha maduka ya dawa muhimu yana wahudumu wenye sifa,ili wananchi wawe na uhakika na dawa wanazonunua,"amesema.

Kaimu Meneja wa TMDA kanda ya Ziwa Mashariki,Venance Burushi amesema mamlaka hiyo imejipanga kuendelea kutoa elimu na kuhakikisha wamiliki wanazingatia matakwa ya sheria.

Amesema lengo la TMDA ni kuhakikisha dawa zote zinazotumika kwa binadamu na mifugo zinakuwa salama, zenye ubora na zinatumika kwa usahihi.

"TMDA inatambua changamoto ya upatikanaji wa maduka yenye wataalam maeneo ya vijijini.Hivyo tunatoa wito kwa wamiliki kushirikiana nasi kupata elimu ya kisheria na tutazidi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kulinda afya za wananchi,"amesema.

TMDA pia imesisistiza wamiliki wa maduka ya dawa wafuate Sheria ya dawa na vifaa tiba ya mwaka 2019,huku ikihimiza wananchi kutoa taarifa finding wanapoona maduka yanaendeshwa kinyume na taratibu.

Akifungua kikao hicho,Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Deogratius Mtaki amesema kuwa wafanyabiashara hao wamepewa dhamana na Serikali juu ya maisha ya wananchi hivyo ni vizuri kuifanya kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni, miongozo na usimamizi wa maduka ya dawa pamoja na famasi.

Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Deogratius Mtaki alizungumza wakati akifungua kikao kazi kati ya TMDA,wamiliki wa famasi na maduka ya dawa.muhimu wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga.

"Zimekuwepp changamoto mbalimbali zinazotokea katika maeneo yenu na tumekuwa tukipata kesi nyingi kwa baadhi ya maduka ya wenzetu si wote wanafanya kazi kinyume na taratibu zilizowekwa  kwa kuendesha bishara zenu kwa kulaza wagonjwa,kuchoma sindano,kufanya to haraka mambo ambayo ni kinyume na kanuni za uendeshaji wa biashara,"amesema 

Mwisho. 




Post a Comment

0 Comments