DIWANI wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Semeni Mussa Mtoka, amefariki dunia.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amesema Semeni amefariki akiwa Hospitali ya
Cardinal Rugambwa (CRH) Ukonga, jijini Dar es Salaam, leo Machio 31, 2026.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Diwani Semeni. Ni masikitiko kwa sababu ni muda mfupi sana tangu achaguliwe kushika wadhifa huo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana,"amesema Sidde.
Amemwelezea Diwani Mtoka kuwa, ameshika nafasi hiyo kwa vipindi viwili na alikuwa mmoja wa madiwani machachari, wakweli, wawajibikaji na alikuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wanawake na jamii nzima kwa ujumla.
Sidde amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana ukisubiri mwongozo wa ndugu wa marehemu ambapo kesho Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Ilala itakaa kikao cha dharura kuhusu utaratibu wa maziko.
Mkuu wa Wilaya ya Iala, Edward Mpogolo, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha diwani huyo, akimwelezea kama mpambanaji, mchapakazi na aliyekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kuleta maendeleo.
"Tumesikitishwa na kifo hiki. Tunamfahamu, alikuwa mwenzetu katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,"amesema Mpogolo.
Source:
#uhuruonline

0 Comments